Safari za ndege za UN nchini CAR ziko mashakani sababu ya ukata-WFP

18 Disemba 2018

Huduma za kibinadamu zinazotolewa na shirika la ndege za Umoja wa Mataifa (UNHAS) ambalo huwawezesha wahudumu wa misaada kuwafikia maelfu ya watu wenye uhitaji nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ziko hatarini kufungwa kutokana na ukata.

Onyo hilo limetolewa leo na shirika la mpango wa chakula duniani WFP ambalo linasimamia huduma hizo. Shirika hilo limeongeza kuwa UNHAS ambalo linategemea msaada asilimia 100 kutoka kwa wahisani wa kimataifa ili kuendesha operesheni zake linahitaji haraka dol;a milioni 3 ili kuendelea kutoa huduma muhimu katika kipindi cha miezi mitatu ijayo la sivyo safari zake zitalazimika kusitishwa mwezi Januari endapo hakuna fedha zozote za dharura zitakazopatikana. 

Kwa mujibu wa mwakilishi na mkurugenzi wa WFP nchini CAR , Bwana Giancarlo Cirri “Uhitaji wa kuwepo kwa UNHAS ni mkubwa zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote na itakuwa zahma kubwa kwa operesheni za misaada endapo huduma hizo zitafungwa. Tunawaomba wahisani washirika wetu kuokoa operesheni hizi muhimu za kibinadamu nchini CAR.”

CAR imekuwa katika machafuko kwa muda mrefu, barabara si salama na hazipitiki na sehemu kubwa ya nchi haina mawasiliano na mji mkuu Bangui hivyo kulifanya shirika la UNHAS kuwa ndio njia pekee ya usafiri kufika katika maeneo ambayo ni vigumu kuyafikia.

Mfano mwezi Novemba pekee UNHAS lilisafirisha wahudsumu wa misaada zaidi ya 2000, ikiwa ni idadi kubwa kabisa kwa mwezi mmoja tangu shirika hilo lianze safari zake nchini CAR mwaka 2006.

WFP inasema zaidi ya nusu ya watu wote nchini CAR sawa (milioni 2.9) wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku raia mmoja kati ya wanne ametawanywa ndani ya nchi aun je ya nchi kutokana na machafuko yanayoendelea na usalama mdogo.

Tangu Januari hadi Novemba mwaka 2018 WFP imetoa msaada wa chakula kwa watu zaidi ya 800,000 wakiwemo watoto wa kati ya umri wa miezi 6 hadi 23ambao wanasaidiwa na mpango maalumu wa kuepuka utapiamlo.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter