Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi kupitishwa leo

Wakimbizi kutoka Iran, Venezuela, Syria, Afghanistan na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR
UNHCR/UNICEF
Wakimbizi kutoka Iran, Venezuela, Syria, Afghanistan na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR

Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi kupitishwa leo

Wahamiaji na Wakimbizi

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Baraza Kuu la chombo hicho litapitisha mkataba wa kimataifa wa wakimbizi na hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa wale wanaokimbia makwao na nchi zinazowahifadhi, ambazo mara nyingi ni zile maskini zaidi duniani. Siraj Kalyango na maelezo zaidi.
 

Tukio hilo linafanyika saa saba na nusu mchana kwa saa za New York, Marekani ambapo litahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo hotuba kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J.Mohammed na Kamishna mkuu wa shirika la kuhudumia wakimbizi, duniani, UNHCR Filippo Grandi, ambao ndio waandaaji wa mkataba huo, maandalizi yaliyojumusha vikao na wadau zikiwemo nchi wanachama wa Umoja wa Mtataifa.

Halikadhalika kwaya ya wakimbizi, iliyopatiwa jina Pihcintu itatumbuiza ambapo kwaya hii inajumuisha wasichana wakimbizi 32 kutoka nchi 17 zikiwemo Zambia, Uganda, Somalia na Sudan Kusini. Miongoni mwao ni Nyawal kutoka Sudan Kusini ambaye katika video yao maalum anasema.. "huwezi kuona nilichopitia kwa kuniangalia tu. Nilikulia kwenye kambi ya wakimbizi, hivyo ninapoona hizo picha, nafirikia jinsi ambavyo maisha yangu yangaliishia.”

Mkataba wa kimataifa kwa wakimbizi una malengo manne ambayo ni mosi, kupunguza mzigo kwa nchi zinazowahifadhi wakimbizi wengi, pili, kuwawezesha wakimbizi kujitegemea, tatu, kuwezesha wakimbizi kufikia nchi  ya tatu kupitia uhifadhi na njia zingine za kunigia nchini na nne kusaidia juhudi zinazowawezesha wakimbizi kurudi katika nchi walikotokea. 

Mkataba huu unalenga kuimarisha mkataba wa wakimbizi wa mwaka 1951 na mifumo mingine juu ya wakimbizi, haki za binadamu na sheria za kibinadamu.

Akizungumza mkataba huo wa mwaka 1951, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR Volker Türk amesema unalenga haki za wakimbizi na wajibu wa wa mataifa lakini hauzingatii ushirikiano wa kimataifa kwa kwa ujumla. Na hilo ndilo jambo ambalo mkataba mpya wa kimataifa kuhusu wakimbizi unalenga kutatua.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.