Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cambodia kutibu unyafuzi kwa watoto kwa kutumia kitafunwa kinachotengenezwa nchini humo

Watoto wa Cambodia wakipata mlo. Watoto kukosa lishe bora husababisha unyafuzi
World Bank/Masaru Goto
Watoto wa Cambodia wakipata mlo. Watoto kukosa lishe bora husababisha unyafuzi

Cambodia kutibu unyafuzi kwa watoto kwa kutumia kitafunwa kinachotengenezwa nchini humo

Afya

Aina mpya ya biskuti yenye virutubisho ikiwemo samaki, Nutrix, imeanza kutengenezwa nchini Cambodia kwa lengo la kutibu utapiamlo miongoni wa watoto.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo huko Phnom Pehn inasema kuwa mpango huo ni ushirikiano kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhuudumia wakimbizi, UNICEF, taasisi ya taifa ya utafiti Ufaransa, IRD, Chuo Kikuu cha Copenhagen, CU, taasisi ya vyakula Denmark, DCF na serikali ya Cambodia.

Wadau hao kwa pamoja walikuwepo kwenye uzinduzi wa utengenezaji wa Nutrix katika mji mkuu wa Cambodia, Phnom Pehn hii leo na kusema uzalishaji utakuwa ni wa kiwango kikubwa.

Naibu Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Asia Mashariki na Pasifiki, Wivina Belmonte amesema, katika eneo hilo, zaidi ya watoto milioni 5 wenye umri wa chini ya miaka mitano hupata  unyafuzi kila mwaka, ambao ni sababu kuu ya vifo miongoni mwa watoto hao.

Amesema “serikali ya Cambodia inapaswa kupongezwa kwa kupatia kipaumbele suala hili na kwa kuimarisha tiba katika ngazi zote. Cambodia inajiunga na nchi nyingine katika kutengeneza kitafunwa kilicho tayari kutumika.

Naye Waziri wa afya wa Cambodia Profesa Mam Bunheng amesema  “uzinduzi wa uzalishaji wa biskuti hii hapa Cambodia ni hatua muhimu katika kufikia lengo la serikali la kutibu angalau kila mwaka watoto 25,000 wenye unyafuzi,”

Ameongeza kuwa kuanza kutengenezwa kwa Nutrix ni hakikisho la upatikanaji wa bidhaa hiyo inayotengenezwa nchini humo.

UNICEF inasema takribani asilimia 2.6 ya watoto nchini Cambodia wanabainika kuwa na utapiamlo uliokithiri au unyafuzi na njia ya kuwatibu ni ile ya kugawa mlo ambao wanaweza kupatiwa nyumbani na kama si hivyo inalazimika kulazwa hospitali. Hata hivyo utafiti unaonesha kuwa bado  kuna uelewa mdogo wa watoto wanaohitaji matibabu kwa kutumia tiba zinazopatikana kwenye vituo vya afya nchini humo.

Serikali ya Cambodia itagawa Nutrix kutibu unyafuzi kwa watoto wenye umri wa chini  ya miaka 5 waishio maeneo ya ndani zaidi na jamii maskini, na mgao utafanyika kupitia vituo vya afya.

Inakadirwa kuwa nchini Cambodia watoto kati ya 60,000 na 90,000 huhitaji tiba maalum kila mwaka ikiwemo kupitia matumizi vya vyakula vya tiba kama Nutrix.

Vitafunwa vyenye virutubisho ambavyo vinafahamika zaidi duniani kutibu magonjwa kama vile utapiamlo hutengenezwa kwa karanga na huagizwa kutoka nje  lakini UNICEF inasema kuwa “viambato vya Nutrix vinapatikana nchini humo na gharama ya utengenezaji wake ni rahisi kwa asilimia 20 ikilinganishwa na uagizaji.”

 “Kwa kutumia bidhaa ambayo inaendana na mazingira ya nchi na ina ladha ya hapa nchini tunweza kuleta athari chanya katika utapiamlo Cambodia. Hii ni muhimu kwa sababu kando ya asilimia 2.6 ya watoto wenye unyafuzi, watoto wengine asilimia 8 wana utapiamlo wa kawaida na hii ni namba kubwa,” amesema Dkt. Frank Wieringa kutoka IRD, na ambaye amekuwa akifanya kazi na UNICEF, CU na DCF kwa miaka 5 kubuni Nutrix.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.