Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR/UNDP: Heko Myanmar kwa kuidhinisha miradi 35 ya kijamii Rakhine

Mwaka mmoja tangu kuanza kwa ghasia nchini Myanmar raia wa kabila la Rohingya wamekimbilia Bangladesh, ambako UNFPA imekuwepo tangu mwanzo wa mzozo kusaidia wanawake na wasichana
UNFPA
Mwaka mmoja tangu kuanza kwa ghasia nchini Myanmar raia wa kabila la Rohingya wamekimbilia Bangladesh, ambako UNFPA imekuwepo tangu mwanzo wa mzozo kusaidia wanawake na wasichana

UNHCR/UNDP: Heko Myanmar kwa kuidhinisha miradi 35 ya kijamii Rakhine

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la mpango wa maendeleo, UNDP leo wameipongeza serikali ya Myanmar kwa kuidhinisha utekelezaji wa miradi 35 ya kijamii ambayo itasaidia kuboresha maisha ya jamii zilizoathirika na machafuko nchini humo.

Pongezi hizo zimetolewa na msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkurugenzi wa kanda ya Asia na Pacific wa UNDP, Haoliang Xu na naibu mkurugenzi wa kikanda wa UNHCR Bernard Doyle, baada ya kukamilisha ziara yao ya siku 5 nchini Myanmar mwishoni mwa wiki.

Wakiwa Myanmar maafisa hao wa Umoja wa Mataifa walizuru jimbo la Rakhine kuanzia Disemba 10 hadi 12 ikiwemo katika mji mkuu wa Sittwe, ambako walikutana na maafisa wa serikali wa eneo hilo.

Ujumbe huo pia ulitembelea vijiji mbalimbali katika wilaya ya  Maungdaw ambako mashirika hayo mawili yamefanya tathimini kwa miezi mitatu iliyopia kubaini mahitaji ya jamii , kufahamu changamoto zinazowakabili na matarajio yao.

Baadaye walikutana na maafisa wengine wa serikali akiwemo Bi. Daw Aung san Suu Kyi na mawaziri wengine muhimu.

UNHCR na UNDP wamesema miradi hiyo 35 iliyoidhinishwa na aserikali ni sehemu ya duru ya kwanza ya tathimini katika jamii zilizoathirika na mbali ya kuboresha maisha itasaidia kujenga hali ya kuaminiana miongoni mwa jamii na kuchagiza mahusiano bora ya kijamii kawa makundi mbalimbali.

Mashirika hayo yamesisitiza kuwa yataendelea kutekeleza ahadi zao za utekelezaji wa makubaliano ya pande tatu yaliyotiwa saini miezi sita iliyopita miongoni mwao na serikali ya Myanmar.

Na wametoa wito wa kupata fursa zaidi ya kufika katika maeneo yote ya jimbo la Rakhine ili waweze kuisaidia serikali kuweka mazingira bora Zaidi kwa ajili ya kurejea kwa hiyari kwa wakimbizi walioko Bangladesh.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.