Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 3.69 kutoka Ujerumani kuchagiza operesheni za WFP Tanzania

Makazi ya wakimbizi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
UNICEF/Gilbertson V
Makazi ya wakimbizi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

Dola milioni 3.69 kutoka Ujerumani kuchagiza operesheni za WFP Tanzania

Wahamiaji na Wakimbizi

Harakati za shirika la mpango wa chakula duniani, WFP nchini Tanzania za kusaidia wakimbizi na wasaka hifadhi nchini humo kwa mwaka 2018-2019 zimepigiwa chepuo hii leo kufuatia msaada wa Euro milioni 3.25 kutoka serikali ya Ujerumani.

Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania Michael Dunford amenukuliwa kwenye taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo jijini Dar es salaam nchini Tanzania akisema kuwa “WFP inatoa shukrani za dhati kwa mchango huu mkubwa kutoka kwa serikali na watu wa Ujerumani. Ujerumani ni mshirika muhimu wa programu za WFP ambazo hutoa msaada wa chakula ulio muhimu sana kwa wakimbizi waishio nchini Tanzania.”

Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Dkt. Detlef Waechter amesema “nchi yangu inajivunia kuiwezesha WFP kuwahudumia wale walio katika uhitaji ambao wamepata hifadhi nchini Tanzania,” akiongeza kuwa “ni muhimu sana kuweka sawa hali ya kisiasa nchini kwao kabla wakimbizi hawa hawajarudi nyumbani kwao kwa hiyari na usalama.”

Upungufu wa fedha ulilazimisha kupunguzwa kwa mgao wa chakula kati ya Februari, 2017 na Oktoba, mwaka huu, kwa hiyo, kuongezeka huku kwa misaada kutoka kwa wahisani, ikiwemo nchi ya Ujerumani, kumewezesha mgao huo kuanza kutolewa tena katika ukamilifu wake. WFP inaendelea kukusanya fedha ili mgao wa chakula usipunguzwe katika miezi ijayo.

WFP hutoa mgao wa chakula cha kila mwezi unaojumuisha nafaka, kunde, mafuta ya mimea na chumvi na vilevile vyakula vya nyongeza vilivyoongezewa virutubisho kwa ajili ya wajawazito walio hatarini na wanawake wanaonyonyesha, watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, watu wenye utapiamlo wanaoishi na VVU/UKIMWI na wagonjwa waliolazwa hospitali.

Halikadhalika shirika hilo hugawa biskuti zenye kutoa wanga wa kiwango cha juu pia hugawiwa kwa wakimbizi walio katika vituo vya muda.
Tanzania inawahifadhi takribani wakimbizi 290,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, hasa katika kambi za wakimbizi za Nduta, Nyarugusu na Mtendeli katika Mkoa wa Kigoma, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Zaidi ya asilimia 70 ya wakimbizi hawa wanatoka Burundi, na waliobaki wanatoka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.