Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 5 tangu kuzuka vita Sudan Kusini, hatma ya watoto 15,000 mashakani

Mtoto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya muda ya kulinda raia huko Bentiu nchini Sudan Kusini.
UNICEF/Holt (file)
Mtoto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya muda ya kulinda raia huko Bentiu nchini Sudan Kusini.

Miaka 5 tangu kuzuka vita Sudan Kusini, hatma ya watoto 15,000 mashakani

Amani na Usalama

Watoto 15,000 wametenganishwa na familia zao au hawajulikani waliko miaka mitano tangu kuanza kwa mzozo nchini Sudan Kusini, limesema shirika la Umoja wa Matiafa la kuhudumia watoto, UNICEF katika taarifa yake iliyotolewa leo.

Hii ni sauti ya mmoja wa watoto nchini Sudan  Kusini ambao wametengana na familia zao na hapa anaonekana akichora mchoro akisema huyu ni mama yangu na baba yangu, sjiawaona tangu mwaka 2016.

Taarifa ya UNICEF inasema kuwa watu milioni 4 wamefurushwa makwao, wengi wao wakiwa ni watoto ambapo UNICEF na wadau wameunganisha takribani watoto 6,000 na wazazi au walezi wao.

UNICEF imesema watoto waliotenganishwa au walio pekee yao wanakabiliwa na hatari ya ukatili, unyanyasaji na kutumikishwa na kwa mantiki hiyo kuwaunganisha na familia ni kipaumbele cha haraka.

Michael Char anafanya kazi na UNICEF nchini Sudan Kusini na anahusika na harakati za kuwakutanisha wanafamilia ambapo anasema

(Sauti ya Michael Char)

 “Kuna kazi nyingi inafanyika katika kuzitafuta na kuunganisha wanafamilia, wakati mwingine inachukua hata miaka, wakati tukimpata mtoto ambaye ametenganishwa na familia, tunaketi naye na kumuuliza maswali mengi, tunawapiga picha na kuzituma kwenye kanzidata ya taifa sio kazi rahisi.”

UNICEF inasema hata baada ya kuwakutanisha na familia nusu ya watoto hao ikiwa ni watoto 3,000 wanahitaji msaada na hivyo idadi ya watoto wanaohitaji msaada imefikia 18,000.

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.