Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vuta nikuvute barazani kuhusu mpango wa Iran wa nyuklia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijadili mpango wa Nyuklia wa Iran. 12 Desemba 2018
UN Photo/Manuel Elías
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijadili mpango wa Nyuklia wa Iran. 12 Desemba 2018

Vuta nikuvute barazani kuhusu mpango wa Iran wa nyuklia

Amani na Usalama

Mkuu wa masuala ya siasa katika Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo leo akiwasilisha ripoti ya pili ya mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa maazimio namba 2231 lililowekwa mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran amelieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa nchi hiyo inaendelea kutekeleza ahadi zake kuhusu Nyuklia.

Akiwasilisha ripoti hiyo ya sita kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, DiCarlo amesema kuwa Katibu Mkuu anapokea uthibitisho wa utekelezaji wa washiriki wote na kwamba, "ni muhimu kuwa mpango unaendelea kufanya kazi kwa washiriki wote ikiwemo faida za kiuchumi kwa watu wa Iran”

Mkutano huu umekuja katika kipindi ambapo kuna mvutano mkubwa kati ya Iran na Marekani ambapo mapema mwezi huu, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marekani Mike Pompeo alisema kuwa Iran imekiuka makubaliano namba 2231 baada ya kujaribu silaha zake za makombora ya masafa ya kati.

Mwezi Mei, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kujiondoa katika makubaliano na akatangaza kuweka vikwazo vipya.

Rosemary A. DiCarlo, Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama
UN/Eskinder Debebe
Rosemary A. DiCarlo, Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama

Rosemary DiCarlo amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasikitishwa na Marekani kurejesha vikwazo ambavyo tayari vilikuwa vimeondolewa akisema kuwa,”Katibu Mkuu anaamini kuwa mambo ambayo hayahusiani moja kwa moja na mpango yanatakiwa kutatuliwa bila kuingilia makubaliano na hatua zilizofikiwa.”

Hata hivyo amesema Katibu Mkuu wa anaitaka Iran izingatie kwa umakini, kutatua, malalamiko ambayo yanatolewa na nchi wanachama kuhusu shughuli za Iran kuhusiana na mambo yaliyozuiliwa.

DiCarlo amemalizia kwa kusema kuwa, kwa Guterres mpango uko pale pale, na akatoa wito kwa nchi wanachama, mashirika ya kikanda na kimataifa kutekeleza mpango na kuepuka matendo ambayo yanaweza kuudhoofisha.

Wajumbe wa Baraza la Usalama nao watoa maoni yao

Balozi Serge Christiane, mwakilishi wa ujumbe wa Muungano wa Ulaya kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza kwenye kikao cha leo amesema, “IAEA katika ripoti 13 mfululizo imethibitisha kuwa Iran inaendelea kutekeleza makubaliano yake kuhusu Nyukilia na kwa kuwa Iran inaendelea na mwenendo huo, EU itaendelea na ahadi yake ya kutekeleza makubaliano”

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje ya Marekani Michael Pompeo ambaye pia ameshiriki mkutano huo amesema,” Iran imetumia vibaya nia njema ya mataifa na pia imekiuka maazimio ya Baraza la Usalama kwasababu ya kiu yake ya silaha za nguvu”

Pompeo akasisitiza kuwa “Umoja wa Mataifa hautalivumilia hili” na kwamba “hakuna nchi yoyote inayotafuta amani na mafanikio mashariki ya kati ambayo inatakiwa kuvumilia hali hii”

Balozi Karen Pierce, Mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama
UN /Loey Felipe
Balozi Karen Pierce, Mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama

JCPOA si leseni kwa Iran kufanya mambo  yasiyofaa- Uingereza

Balozi Karen Pierce, mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza kuwa kwa Iran kuenenda sawa na mpango wa JCPOA siyo leseni ya kufanya mambo mengine yasiyofaa yawe yanahusu nyukilia ama la.

“Iran haitakiwi kutegemea kuboresha mahusiano yake na dunia au kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na usalama wakaati ikifuata mkondo inaoenda nao”

Naye Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Vasily Nebenzya amesema, “sasa tuko njiapanda, yaani pale ambapo mwanachama mmoja wa Baraza la Usalama waziwazi anakataa kutekeleza makubaliano ambayo yeye mwenyewe aliyapitisha lakini anajaribu pia kuwaadhibu wanachama wengine wote ambao wanatekeleza maamuzi ya baraza na kamati ya JCPOA”

Iran haikukaa kimya, yajibu hoja

Akijibu hoja hizo, mwaklishi wa kudumu wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa, balozi  Eshagh AI Habib amesema, “la kushangaza ni Marekani, ambaye yeye mwenyewe anakiuka makubaliano kisha leo anailaumu Iran kwa kuyakiuka makubaliano haya,” akiongeza kuwa “tulichokisikia leo ni mfululizo mwingine wa uongo, ulaghai, na taarifa za upotoshaji za Marekani.”

Makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa nyukilia wa Iran JCPOA yalifikiwa mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari mosi, 2016.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.