Wataalamu wa UN walaani hatua ya Belarus kunyonga watu watatu licha ya ombi kuwa isifanye hivyo

12 Disemba 2018

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamelaani kitendo cha Belarus cha kuendelea kutumia hukumu ya kifo, ikidhihirisha kuwa taifa hilo limekaidi ombi la kamati ya haki za binadamu la kutowanyonga watu watatu ambao ni Alessei Mikhalenya, Semyon Bereahnoi na Igor Gershankov.

Wataalam hao kupitia taarifa yao iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, wamelaani kitendo hicho kufuatia taarifa kwamba watu hao watatu tayari wamenyongwa hadi kufa wakati malalamiko yao yakiwa bado yanashughulikiwa na kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Mwenyekiti wa kamati ya hiyo, Yuval Shany, amesema kuwa hatua ya Belarus ya kuendelea kupuuza utaratibu wa kamati hiyo pamoja na hatua za muda ilizotoa ni jambo ambalo halikubaliki. “Ukweli ni kwamba kushindwa katika mukhtadha wa kesi kama hizo zenye hukumu ya kunyongwa ambazo kamati inazichukulia kama haki ya juu hauvumiliki,”amesema.

Naye Anais Marin, Mtaalam Maalum kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Belarus, amesema kuwa bila kujali makosa waliyotenda, kama binadamu, watu hao  walipaswa kuwa na haki ya kuishi na kuzifanya familia zao zisijue  wakati na mazingira ya vifo vya watu wao na pia kushindwa kurejesha miili yao kwa familia kunaleta  machungu sana kwa familia hizo.

Taarifa zisema kuwa Mikhalenya, aliyepatwa na hatia ya mauaji na kuhukumiwa kifo machi 2017, alinyongwa mei 15 mwaka huu. 
Berezhnoi na Gershankov wote walipatikana na hatia ya mauaji Julai 2017 na wanaripotiwa kunyongwa haid kufa tarehe 19 mwezi huu wa Novemba .

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter