Guterres afananisha kutotimiza mkataba wa mabadiliko ya tabianchi na kujiua

12 Disemba 2018

Wakati ambapo majadiliano kuelekea mpango madhubuti wa utekelezaji wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015 yakiendelea kukumbwa na vikwazo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo hii amerejea Katowice, Poland kuwapa changamoto zaidi ya viongozi 100 wa serikali ambao wanakutana katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi COP24 kufikia makubaliano na kuikamilisha kazi.

Guterres amesema, “katika hotuba yangu ya ufunguzi wa mkutano huu wiki moja iliyopita, nilionya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanakimbia kwa kasi zaidi kuliko sisi na kwa hivyo mkutano huu wa Katowice bila vikwazo unaopaswa kufanikiwa kama eneo muhimu la kuirejesha hali kama ilivyokuwa awali”

Tangu Desemba pili , mkutano huu umewaleta pamoja maelfu wakiwemo watoa maamuzi, watetezi na wanaharakati wa masuala ya tabianchi wakiwa na lengo moja muhimu la kuidhinisha kile kilichopitishwa katika makubaliano ya Paris mwaka 2015 ambapo nchi zilikubaliana kuzuia joto la dunia liwe chini ya nyuzi joto 2°C na karibu na nyuzi joto 1.5°.

Zikiwa zimesalia siku tatu za majadiliano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasikitika kuwa pamoja na kuwa hatua imepigwa katika nyaraka za majadiliano, lakini bado kuna mengi hayajafanywa.

Barafu ikiyeyuka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Hali hii inaweza kuongeza kina cha bahari.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Barafu ikiyeyuka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Hali hii inaweza kuongeza kina cha bahari.

“Mambo kadhaa ya kisiasa hayajatatuliwa. Haishangazi tunatambua ugumu wa kazi hii lakini muda unatutupa mkono,” Guterres ameonya akikumbushia ripoti maalumu ya mabadiliko ya tabianchi iliyotolewa mwezi Oktoba mwaka huu na na jopo la kimataifa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi IPCC.

“Kwa siku 10 wengi wenu mmefanya kazi kwa muda mrefu, kazi ngumu na nataka kuwapongeza kwa hilo lakini tunahitaji kuongeza juhudi kufikia makubaliano ikiwa tunataka kweli kufuata maazimio ya Paris, " amesema Guterres.

 

Amekumbusha wajumbe kuwa "ninatambua wengine mtahitaji kufanya maamuzi kadha magumu ya kisiasa lakini huu ni wakati wa kufikia makubaliano. Ni vigumu kuwaelezea wale ambao wanateseka na na mabadiliko ya tabianchi kwamba tumeshindwa kupata hatua zinazotakiwa kuchukuliwa. Tufanye kazi pamoja tumalize kazi hii. Hii inamaanisha kujitolea na itatufaidisha sisi sote. Kuipoteza nafasi hii ya Katowice itakuwa siyo tu ni kinyume na maadili bali itakuwa ni kujiua.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter