Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa popote ulipo unaweza kuona msitu wowote duniani bila gharama

Picha ya setilaiti ya NASA ikionyesha  sehemu za milima na jangwa la Taklamakan China
USGS/NASA
Picha ya setilaiti ya NASA ikionyesha sehemu za milima na jangwa la Taklamakan China

Sasa popote ulipo unaweza kuona msitu wowote duniani bila gharama

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kitendo cha mtu kuweza kuona misitu au miti sasa inatarajiwa kuwa rahisi zaidi kutokana na teknolojia mpya ya kisasa iliyobuniwa kwa ushirikiano kati ya shirika la anga za juu la Marekani, NASA na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO na wadau wengine wakiwemo Google.

Teknolojia hiyo Collect Earth Online au CEO ipatikanayo kwenye mtandao wa intaneti imeboresha mbinu ya awali ambayo ilikuwa inawezesha mtu kuona takwimu ya matumizi ya ardhi lakini sasa itakuwa na picha pia za setilaiti.


Taarifa ya FAO iliyotolewa leo mjini Katowice, Poland, inaeleza kuwa CEO ni wavuti http://collect.earth/  isiyohitaji malipo yoyote ambapo mtumiaji anaweza kukagua sehemu yoyote ile duniani kwa kutumia takwimu za setilaiti na kupata majibu haraka na kwa urahisi


Mkuu wa kitengo cha FAO kinachohusika na sera pamoja na usimamizi wa misitu, Mette Wilkie,  amesema,  “ubunifu huu unawezesha  kukusanya  data mpya kuhusu mazingira yetu na mabadiliko yoyote yale katika njia nzuri na rahisi kwa kutumia watalam wa kawaida ambao wanaelewa vizuri sehemu zetu pamoja na ekolojia.”


Naye  Meneja wa mpango wa NASA wa SERVIR Global Progam, Dan Irwin, amesema kuwa CEO inahusiana na picha za setilaiti na hutumiwa kukusanya data kuhusu dunia. 
Ameongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa data za miongo minne za picha za setilaiti “inaweza kusaidia nchi nyingi duniani kuona na kupanga upya ramani za misitu yake.”
FAO inasema ufuatiliaji wa misitu iliyoko duniani ni kazi ambayo inazidi kuwa na changamoto lakini pia yenye tija, “wakati huu ambapo umuhimu wake kwa mbao na mafuta unaimarishwa pia na uelewa wa dhiam yake katika kuhifadhi hewa ya ukaa, udhibiti wa wadudu na kilimo.”
Imetolea mfano kitengo cha FAO cha udhibiti wa panzi  ambacho kinatumia mbinu iitwayo FORIS kwa ajili ya kuimarisha utabiri na udhibiti wa baa la wadudu hao hatari.