Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cameroon acheni kukandamiza wananchi wanaotekeleza haki zao – UN

Familia ya wakimbizi kutoka Cameroon ikiwa nje ya kibanda chao katia makazi ya Adagom, kusini mashariki mwa Nigeria.
UNHCR/Roqan Ojomo
Familia ya wakimbizi kutoka Cameroon ikiwa nje ya kibanda chao katia makazi ya Adagom, kusini mashariki mwa Nigeria.

Cameroon acheni kukandamiza wananchi wanaotekeleza haki zao – UN

Amani na Usalama

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameonyesha  wasiwasi wao kufuatia msako unaofanyika dhidi ya waandamanaji nchini Cameroon, baada ya Rais Paul Biya kuchaguliwa tena kuongoza nchi hiyo, hivyo wametaka uhuru wa kujieleza, kukusanyika kwa amani pamoja na uhuru wa kujiunga kwenye vikundi uheshimiwe.

Wataalam hao wamesema hayo kupitia taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na ofisi ya  haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa wakisema kanuni za kimataifa za haki za binadamu zinampatia kila mtu haki ya mtu kushiriki katika maaandamano ya amani na uzuiaji wowote wa haki ya kukusanyika na pia ya kujieleza ni sharti ufuate sheria na usivuke kipimo.
Tamko hili la wataalamu limechochewa na taarifa za mwezi uliopita zinazoashiria kipindi cha mazingira magumu kwa makundi ya kiraia, vyama vya kisiasa, na watu wanaokosoa serikali kutokana na matokeo ya uchaguzi mkuu, ambapo rais Biya aliibuka na ushindi, wataalam wakisema kuwa hatua dhidi ya wakosoaji zinaonekana kama zinabinya wakosoaji wa serikali ili kuwazuia kutoa maoni yao bila woga wowote.


Wataalam hao wamesema,  “uzuiaji ambao umewekwa juzi na serikali ya Cameroon dhidi ya haki ya kukusanyika kwa amani na kujieleza yaonekana haukutilia maanani kanuni  za kimataifa ambazo Cameroon iliziridhia.”  


Wamesisitizia  sheria ya nchi hiyo dhidi ya ugaidi ya mwaka  2014 na kusema  isitumike kuzuia maandamano ya amani ambayo yameandaliwa na  vyama vya kisiasa wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kipindi cha kuwekwa korokoroni kinaweza kuongezwa kutoka saa 48 hadi siku 15 na mamlaka ya kusimamia kesi ikahamishiwa kwa mahakama za kijeshi.
Wataalam hao huru ambao waliteuliwa na Baraza la haki za binadamu, mapema walielezea wasiwasi wao kwa wakuu nchini Cameroon wakilalamikia tafsiri pana ya ugaidi kama,  “uvurugaji wa huduma za kawaida za umma,” kuwa kunaweza kutumiwa vibaya  kwa kupiga marufuku mikutano ya amani.  


Wamesema hadi  leo bado shaka na shuku zao hazikuwa zimepatiwa jibu hadi leo na wametaka serikali ya Cameroon iheshimu sheria zinazohusu kuandamana ambazo zinawataka waandaaji kuarifu mapema mamlaka  siku saba kabla ya siku ya maandamano.