Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndoa za utotoni bado zawanyemelea watoto wa kike Malawi- Ripoti

Balozi mwema wa UN Emma Watson alipotembelea shule ya sekondari ya Mtakataka katika wilaya ya Dedza kuwasikiliza Stella Kalilombe na Cecilia Banda ambao ndoa zao zilibatilishwa wakarejea shuleni kupata elimu.
UN Women/Karin Schermbrucker
Balozi mwema wa UN Emma Watson alipotembelea shule ya sekondari ya Mtakataka katika wilaya ya Dedza kuwasikiliza Stella Kalilombe na Cecilia Banda ambao ndoa zao zilibatilishwa wakarejea shuleni kupata elimu.

Ndoa za utotoni bado zawanyemelea watoto wa kike Malawi- Ripoti

Wanawake

Nchini Malawi, licha ya mafanikio  yaliyopatikana katika kupunguza ndoa za utotoni kwa watoto wa kike, bado mtoto mmoja kati ya wanne anaozwa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Benki ya Dunia imetoa takwimu hizo katika ripoti yake ya ufuatiliaji wa uchumi wa Malawi, MEM ikipatiwa jina Kuwekeza katika Elimu ya Msichana.

Toleo hilo la nane linaonyesha kuwa pamoja na kuozwa katika umri mdogo, watoto watatu wa kike kati ya 10 wanajifungua mtoto wao wa kwanza kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Akizungumzia mwelekeo huo, Mkuu wa Benki ya Dunia nchini Malawi, Greg Toulmin amesema “gharama ya ndoa za utotoni na ukosefu wa elimu miongoni mwa watoto wa kike ni upotezaji wa fursa kubwa kwa watoto, jamii na uchumi.”

Benki ya Dunia inasema kuelimisha watoto wa kike na kutokomeza ndoa za utotoni nchini Malawi kunaweza kuchangia faida kubwa za kiuchumi ikiwemo dola nusu bilioni zinazoweza kupatikana ifikapo mwaka 2030 iwapo watoto hao watakwenda shule na kuajiriwa au kujiajiri na hatimaye kuwa na kipato cha kuwawezesha kununua bidhaa na hivyo kuchangia kwenye  uchumi wa nchi.

Sambamba na hilo, “iwapo wanawake ambao waliolewa wakiwa watoto wangalicheleweshewa ndoa zao, mapato yao ya kilwa mwaka yanakadiriwa kuwa yangalikuwa dola milioni 167.”

Kwa mantiki hiyo basi ripoti hiyo inapendekeza hatua kadhaa ikiwemo kuweka mbinu ambazo zitawezesha watoto wa kike kusalia shule muda mrefu na kumaliza masomo, kuboresha mazingira ya shule kwa wasichana na kutokomeza ndoa za utotoni sambamba na watoto wa kike kujifungua mapema watoto wenzao.