Upandaji miti kutoka Dakar hadi Djibouti ni mradi wa aina yake- UNCCD

12 Disemba 2018

Mradi wa kupanda kutoka Dakar hadi Djibouti uliopatiwa jina la Ukuta wa Kijani, ni moja ya mwamko unaoleta matumaini na unaohitajika haraka katika zama hizi,” amesema mwanasayansi mkuu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na uharibifu wa ardhi, UNCCD Dkt. Barron Joseph Orr.

Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kandoni mwa mkutano wa nchi  wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP24 unaoendela Katowice, Poland,  Bwana Orr amesema mradi huo unaoongozwa na bara la Afrika unalenga kupanda miti umbali wa kilometa 800 utakaozunguka upana wa bara hilo kwa ajili ya kubadilisha maisha ya mamilioni ya watu wanoishi kwenye maeneo yaliyo hatarini kugeuka jangwa  na wanaokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Ameelezea pia baadhi ya sababu za uharibifu wa ardhi akisema kuwa ongezeko la watu linachochea mahitaji na matumizi ya ardhi kwa njia isiyo endelevu na pia“inaweza kusababishwa na mambo mengi, kwa mfano umaskini ambapo unagundua kuwa unalazimika kuwalisha watoto na hivyo kulisha mifugo eneo moja kwa muda mrefu au upanzi wa mimea mingi au namna tunavyoweka mbolea au pembejeo zingine zinaweza athiri rutuba ya udongo na hiyo kusababisha uharibifu.”

UNDP Chad/Jean Damascene Hakuzim
Watoto katika eneo la Merea nchini Chad wakipanda miti kama nija mojawapo ya kukabiliana na kuenea kwa jangwa nchini humo

Amesema kuwa licha ya kwamba uharibifu wa ardhi unashuhudiwa katika nchi zote duniani, “ni vigumu kutaja nchi ambako uharibifu wa ardhi haupo, upo kila mahali lakini unajitokeza kwa njia mbalimbali ila katika maeneo kavu ni dhahiri kuwa hali ni mbaya zaidi Afrika hususan ukanda wa Sahel lakini kuna matukio Asia ya Kati na Amerika Kusini. Sio tukio ambalo linatokea katika bara moja au nyingine."

 Kwa mantiki hiyo ametaja mradi huo wa ukuta wa kijani ambao ulianzishwa mwaka 2017 ili kukabiliana na uharibifu huo kuwa ni zaidi ya kupanda miti kwani unajumuisha mazingira , masuala ya kijamii na kiuchumi na mikakati ya kitamaduni kwa ajili ya kuimarisha maisha ya watu ambako uharibifu wa ardhi umeshuhudiwa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud