Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa kimataifa wa uhamiaji wafunga pazia ukiridhiwa na nchi zaidi 160

Louis Arbour,Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa.
UN Photo/Rick Bajornas)
Louis Arbour,Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa.

Mkutano wa kimataifa wa uhamiaji wafunga pazia ukiridhiwa na nchi zaidi 160

Wahamiaji na Wakimbizi

Baada ya nchi zaidi ya 160 kupitisha kwa kauli moja mkataba wa kihistoria wa kimataifa kwa ajili ya kushughulikia suala la uhamiaji kwa njia salama na ya mpangilio, afisa wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya uhamiaji ameelezea uungwaji mkono wa mkataba huo na jumuiya ya kimataifa kuwa ni ushirikiano wa kimataifa katika kilele chake.

Louise Arbour ambaye ni mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kufunga mkutano huo amesema “Kwa kufanya hivyo serikali zimeahidi kuzingatia mfumo huo kwa misingi ya kweli na sio hadithi na kwamba mkataba huu utalinda maslahi ya taifa na kuwezesha ushirikiano bora, kama lilivyo jina lake mkataba huu imeundwa kwa mantiki ya kuimarisha usalama na mpango wa kudhibiti suala la uhamiaji na kupunguza hatari na njia zisizosalama za kusafirisha wahamiaji.”

Pia amesema utahakikisha kutumia fursa zote za faida za uhamiaji na kupambana na changamoto zake.

Msingi wa mkataba huo wa kimataifa ni kusisitiza  kwamba wahamiaji kila mahali ni lazima watendewe haki na utu. Bi. Arbour ametoa wito kwa serikali ambazo hazijaridhia mkataba huo kufikiria upya misimamo yao, na kuongeza, “Ninawataka muusome kwa makini na bila shaka kuwa na maoni yenu."

Akizukumbusha nchi zilizoendelea kuhusu faida ya uhamiaji wa kimataifa Bi. Arbour amesema  “wanakidhi mahitaji ya kiuchumi kwa kukuza nguvu kazi, na kwa upande mwingine wakati nchi zinahifadhi wakimbizi na watu walio katika taharuki ya kupata hifadhi  ni lazima zisaidiwe na kupongezwa kwa kuifanya dunia kuwa mahali bora pa kuishi kwetu sote”

katibu Mkuu  huyo wa mkutano pia ameishukuru  serikali ya Morocco kwa kuwa mwenyeji na kuwezesha mkutano huo wa kihistoria wa wahamiaji kufanyika Marrakesh Morocco na kusema ,“tunaondoka Marrakesh tukiwa tumejawa na nguvu na hamasa.Tukiwa na mkataba huu wa kimataifa tuna fursa ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kuhusu uhamiaji.”

 

Lango la kuingilia katika jumba la mkutano wa uhamiaji Marrakesh, Morocco.
UN Photo/Abdelouahed Tajani
Lango la kuingilia katika jumba la mkutano wa uhamiaji Marrakesh, Morocco.

 

Watu zaidi ya 2000 wamehudhuria mkutano huo wa kimataifa wakiwemo maafisa wa serikali, wawakilishi wa makampuni ya biashara , jumuiya za wafanyakazi, asasi za kiraia, mameya na wadau wengine wengi ambao wana jukumu muhimu la kuhakikisha kwamba uhamiaji unadhibitiwa kwa njia ambayo inaleta faida kwa wote.

 

Mkataba uliopitishwa lazima ufuatiwe na utekelezaji

Waziri wa mambo ya nje wa Morocco, wenyeji wa mkutano, amesisitiza umuhimu wa nchi yake kwa ushirikiano wa kimataifa katika kushughulikia changamoto ya sasa ya uhamiaji. Bwana  Nasser Bourita, amewaambia waandishi wa habari kwamba nchi wanachama wameonyesha kwamba suala la uhamiaji linaunganisha zaidi ya kutenganisha.Akiongeza kuwa kupitishwa kwa mkataba huo ni hatua ya kwanza ambayo ni lazima ifuatiwe na utekelezaji , akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kukusanya nguvu zao katika suala hili.

 

Ellen Johnson Sirleaf,Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu kuhusu Uhamiaji wa kimataifa barani Afrika kwenye mkutano kuhusu uhamiaji Marrakesh, Morocco.
UN Photo/Mark Garten)
Ellen Johnson Sirleaf,Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu kuhusu Uhamiaji wa kimataifa barani Afrika kwenye mkutano kuhusu uhamiaji Marrakesh, Morocco.

Mkataba huu utatoa mtazamo tofauti:Sirleaf

Akitoa maoni kuhussu mkataba huo wa uhamiaji utakavyokuwa na athari barani Afrika, rais wa zamani wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf amesema, “Mkataba huu utasitisha madhila waliyokuwa wanayapitia Waafrika, idadi ndogo ya waliojaribu kuvuka mipaka kinyume cha sheria. Afrika sasa itaweza kupitisha sera ambazo zitahakikisha kwamba watafanya juhudi zaidi ya ambavyo tayari wanafanya kuhakikisha kwamba wanainua uchumi na kushinda vita dhidi ya umasikini ili kuwafanya vijana wetu kusalia nyumbani.”

Bi. Sirleaf ambaye alikuwa mwenyekiti wa mjadala wa ngazi ya juu kuhusu uhamiaji barani Afrika amekariri kwamba mkataba huo utaziwezesha nchi za Afrika kutafuta njia za kuhakikisha kwamba watu wanaovuka mipaka wanatendewa ubinadamu na utu wanaostahili, “nadhani mkataba utaiwezesha Afrika na dunia nzima kwa ujumla kuliona suala la uhamiaji katika jicho tofauti ambalo ni chanya na linalochangia katika maendeleo na kuchagiza ushirikiano baina ya nchi.”

 

Teknolojia  kama nyenzo.
ITU
Teknolojia kama nyenzo.

 

Teknolojia kama nyenzo ya mabadiliko

Wakati wa kukunja jamvi la mkutano huo hii leo masuala muhimu yaliyojadiliwa ni ushirikiano na miradi ya ubunifu. Mkurugenzi kituo cha Brookings kilichopo Doha, Tarek Yousef, ameelezea jukumu la ubunifu wa  kiteknolojia katika kusaka suluhu mujarabu la changamoto ya wahamiaji. Amesema kwa kutumia program maalumu za kiteknolojia kutawawezesha wahamiaji kujua haki zao kisheria, hali ambayo itawasaidia kupambana na ubaguzi na manyanyaso na ameongeza kuwa hili zaidi liko mikononi mwa jamii za wenyeji na viongozi wa maeneo husika kwani amesema “Huitaji Marais wa nchi kuidhinisha hili , unachohitaji ni wadau muafaka kufanya kazi inayotakiwa na kuondoa vikwazo.