Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa Sweden kuleta nuru ya afya kwa wakazi wa Magharibi mwa mto Nile Uganda

Mtoto akiwa amebebwa na mamamke katika kituo cha afya nchini Mali.
UNICEF/UN0186355/Njiokiktjien
Mtoto akiwa amebebwa na mamamke katika kituo cha afya nchini Mali.

Msaada wa Sweden kuleta nuru ya afya kwa wakazi wa Magharibi mwa mto Nile Uganda

Afya

Baada ya Sweden kupitia shirika lake la misaada ya maendeleo ya kimataifa, SIDA kuitikia wito wa usaidizi wa fedha wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef nchini Uganda, sasa kuna matumaini makubwa ya kwamba huduma za afya kwa wajawazito, barubaru na watoto wachanga zitaimarika. 

Mchango huo wa Sweden unalenga kunufaisha watoto wenyeji na wakimbizi takriban milioni moja katika eneo la Magahribi ya Mto Nile kwa kuwapatia fursa ya kufikia huduma bora za afya.

Utatumiwa kujenga uwezo wa wahudumu wa afya, kununua vifaa afya hospitalini, maji na vifaa vya kujisafi  kama sehemu ya njia za kuinua mtindo wa huduma za afya ya uzazi katika jamii za wenyeji na wakimbizi.

Mradi huu utanufaisha wilaya za Adjumani, Arua, Koboko, Maracha, Moyo, Nebbi, Packwach, Yumbe na Zombo.

Mwakilishi wa shirka la Umoja wa Matifa la Kuhudumia watoto, UNICEF Uganda Dkt. Doreen Mulenga, amesema mchango huu wa Sweden unaisaidia kufikia ndoto yake ya kusaidia serikali ya Uganda kuimarisha huduma za afya ya watoto, barubaru na wajawazito katika eno la Magharibi ya Mto Nile.

Watoto 480,000 walio chini ya umri wa miaka mitano, na barubaru 460,000 ndio wanalengwa wakuu wa kunufaika na mchango huu.