Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa UN walenga kusaidia wasyria na jamii zinazowahifadhi

Watoto wakiwa katika kambi ya Rukban nchini Syria. Ni wakimbizi wa ndani mwa nchi.
WFP
Watoto wakiwa katika kambi ya Rukban nchini Syria. Ni wakimbizi wa ndani mwa nchi.

Mpango wa UN walenga kusaidia wasyria na jamii zinazowahifadhi

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau, leo yamezindua mpango wa kikanda wa mwaka 2019-2020 kwa ajili ya kuwajengea stahamala wakimbizi wa Syria na nchi zinazowahifadhi.

Ukipatiwa jina la 3RP, mpango huo wenye thamani ya dola bilioni 5.5 unatarajiwa kusaidia juhudi za Uturuki, Lebanon, Jordan, Misri na Iraq kukabiliana na athari mbaya za mzozo wa Syria.

Taarifa ya mashirika hayo ikiwemo lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na la mpango wa maendeleo, UNDP imesema nchi jirani zimekuwa karimu katika kuwahifadhi wakimbizi tangu mzozo wa Syria ulipoanza, kwa kuwawezesha kusaka hifadhi, ulinzi, kupata huduma za umma na kuchangia katika uchumi licha ya athari hasi dhidi ya uwepo wao.

Licha ya hayo, mashirika hayo kupitia taarifa yao yamesema kuhifadhi wakimbizi hao kunazua changamoto kwani wakimbizi milioni 5.6 wamesajiliwa katika ukanda huo na watoto milioni moja wamefurushwa.

Huku watoto hao wakitajwa kuzaliwa katika mazingira ambamo kunashuhudiwa umaskini na ukosefu wa ajira, ndoa za mapema na ajira za utotoni zinafanyika, na elimu sio hakika.

Mashirika hayo yametoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia katika juhudi za mpango huo wa 3RP kwani jamii zinazowahifadhi waSyria zinakabiliwa na changmoto za kiuchumi na kijamii.

Ifikapo mwaka 2019 mpango huo wa 3RP unatarajiwa kusaidia watu milioni 9 katika nchi tano kwa misaada kwenye maeneo kama vile ulinzi kwa wakimbizi, kuandikisha watoto shule, kuimarisha huduma muhimu na fursa za kiuchumi hususan kwa wanawake.

Wakati mpango huo ukizinduliwa shrika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema kwa sasa watu milioni 6.5 nchini Syria wana njaa ambapo WFP inafikia watu milioni 3 kila mwezi ikiwemo watu milioni 3.3 wanoishi kambini nje mwa Syria.

Halikadhlika WFP inasaidia watu 81,000 nchini Misri, 47,000 nchini Iraq, 880,000 nchini Jordan, 670,000 nchini Lebanon na milioni 1.5 nchini Uturuki.