IOM yapongeza hatua ya kuidhinishwa kwa mkataba kuhusu uhamiaji.

Sanamu katika jumba la mikutano Marrakesh, Morocco. Disemba 2018
UN Photo/Mark Garten)
Sanamu katika jumba la mikutano Marrakesh, Morocco. Disemba 2018

IOM yapongeza hatua ya kuidhinishwa kwa mkataba kuhusu uhamiaji.

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa mataifa la uhamiaji-IOM-limepongeza kuidhinishwa kwa mkataba kuhusu uhamiaji na kuiita hatua hiyo kama ya kihistoria na mafanikio kwa jamii ya kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa mjini Marrakesh, Morocco na Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Antonio Vitorino,ambaye amesema kuwa, “uhamiaji ni suala muhimu enzi hizi na kuidhinishwa kwa mkataba huo kwa kauli moja na wanachama wa Umoja wa Mataifa kutasaidia kupata sera bora na ushirikiano mkubwa katika uhamiaji.”

Ameongeza kuwa mambo muhimu kwenye mkataba huo ni kuwa mataifa yanahitaji uhamiaji ambao una utaratibu mzuri na kuwa hakuna taifa moja linaloweza kufanikisha hilo peke yake.

Msemaji wa IOM Joel Millman, akizungumza na waandishi habari leo mjini Geneva Uswisi, amesema kuwa

“Kuna takriban wahamiaji wa kimataifa milioni 260 duniani na mkataba huu unaweka misingi na azma na uelewano kadhaa baina ya nchi. Hii ni kama  vile masuala ya haki za biandamu, ya kibinadamu, kiuchumi, kijamii, kimaendeleo, mabadiliko ya tabianchi pamoja na usalama ambavyo vinawathiri wahamiaji, mataifa yao asili, wanayopitia na pia jamii zinazowakaribisha.”

Mchakato wa kuidhinisha mkataba huo ulianza miaka miwili iliyopita wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipozungumzia  suala la wimbi la wahamiaji na wakimbizi na matokeo yake ni tamko la New York kuhusu wakimbizi na wahamiaji.