Mradi wa Benki ya Dunia Niger wakomesha hamahama ya wananchi kutokana na ukame

11 Disemba 2018

Wakati mabadiliko ya tabianchi yakiendelea kuwa tishio kwa watu maskini zaidi duniani Benki ya dunia imetangaza kuwekeza dola bilioni 200 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa ajili ya kuweka mazingira bora na kujengea stahamala nchi zilizoathirika. Mojawapo ya nchi ambako Benki ya Dunia imewekeza ni Niger.

Sauti ya Adamou Dan Jah kutoka kijiji cha Garin Madougou, koranko nchini Niger, ni wakati wa jua likichomoza na anaelezea alikozaliwa, akisema kuwa wao ni wakulima na wanategemea kilimo kwa ajili ya kulisha familia na iwapo hamna mazao  basi wanakuwa na wasiwasi.

Akiwa kwenye eneo kavu likiashiria mvua hazijanyesha kwa siku nyingi Dan Jah kupitia video iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Benki ya Dunia anasema

(Sauti ya Dan Jah)

“Wakati tulikuwa wadogo maisha yalikuwa mazuri, lakini mimea tuliyokuwa tukipanda wakati huo haishamiri tena.Tulilazimika kuziacha familia zetu na kuhama, sikuwa na amani, nikiwawaza niliowaacha nyumbani.”

Lakini bwana Dan Jah anasema sasa ana amani tangu kuanza kutekelezwa kwa  mradi wa Benki  ya Dunia wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo walipokea mbegu bora za mtama na miche ya mihogo zinazostahimili ukame na sasa anafurahia kwani shamba limestawi..

(Sauti ya Dan Jah)

“Huhitaji kumwagilia maji mihogo na baada ya mvua mara mbili unaweza kuvuna zao lako na kutokana na mauzo yake, faida inaniwezesha kukidhi mahitaji yangu, mbegu bora za mtama zinasaidia zao kustawi licha ya uhaba wa mvua. Watu hawawazi tena kuhama.”

Anatolea wito jamii ya kimataifa kukubali kuwa mabadiliko ya tabianchi yapo na kulinda vizazi vijavyo kutokana na athari zake mbaya.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud