Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Milima ni muhimu tuilinde kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo

Mkulima akikagua migomba yake kwenye eneo la milima huko Anjouan nchini Comoro. Mabadiliko ya tabianchi  yamekuwa 'mwiba' na kusababisha mmomonyoko wa udongo.
UN Environment/Hannah McNeish
Mkulima akikagua migomba yake kwenye eneo la milima huko Anjouan nchini Comoro. Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa 'mwiba' na kusababisha mmomonyoko wa udongo.

Milima ni muhimu tuilinde kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ni siku ya milima duniani ambapo Umoja wa Mataifa unapigia chepuo  maeneo hayo kwa kaulimbinu milima ni muhimu.

Umoja wa Mataifa kupitia wavuti maalum wa siku hii, unasema kuwa ingawa milima imetajwa katika ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu,  bado milima inasahaulika.

“Kwa kuzingatia dhima muhimu ya milima katika kupatia viumbe vya dunia huduma na bidhaa pamoja na hatari ambazo inakumbana nayo wakati huu wa mabadiliko ya tabianchi, ni vyema tuongeze hatua ili kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wake na kuilinda,” umesema Umoja wa Mataifa.

FAIDA ZA MILIMA

Faida za milima ni lukuki na mosi ni maji kwa kuwa milima ni vilele ambamo kwavyo maji hutiririka ikielezwa kuwa milima ni chanzo cha kati ya asilimia 60 hadi 80 ya maji yote yanayopatikana duniani.

Pili ni faida yake katika kupunguza majanga kwa kuwa ni kimbilio kwa watu wengine pindi majanga yanapotokea. Faida ya tatu ni utalii ikielezwa kuwa “takribani asilimia kati ya 15 hadi 20 ya utalii duniani hufanyika milimani kutokana na maeneo hayo kuwa na tofauti mbalimbali za vivutio, watu wenye ufahamu tofauti na urithi.

Chakula nacho ni miongoni mwa faida za uwepo wa milima ambapo Umoja wa Mataifa unataja vyakula kama vile quinoa, mchele, nyanya na hata viazi, mathalani kwenye vilima vya  Usambara huko mkoani Tanga nchini Tanzania. Halikadhalika milima ni makazi ya watu wa asili ambao wana ufahamu wa kipekee wa kitamaduni, ufahamu ambao ni lulu katika maisha ya sasa.

Ni kwa kuzingatia faida hizo, Umoja wa Mataifa unataka maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya milima duniani yatumike kuangazia harakati ili kuongeza ufahamu wa umuhimu wa milima kwa wanasiasa na watunga sera.

Hii leo shirika la chakula na kilimo duniani, FAO linatumia kampeni kupitia mtandao #Mountainsmatter ili kuchagiza uelewa wa umuhimu wa milima duniani.