Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama hazijatetereka licha ya mitandao ya kijamii kuwa changamoto uendeshaji wa kesi

Dkt. Elifuraha Laltaika, mtaalamu wa jukwaa la kudumu la watu wa asili la Umoja wa Mataifa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili
UN News
Dkt. Elifuraha Laltaika, mtaalamu wa jukwaa la kudumu la watu wa asili la Umoja wa Mataifa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili

Mahakama hazijatetereka licha ya mitandao ya kijamii kuwa changamoto uendeshaji wa kesi

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Licha ya mihemuko ya wananchi na viongozi katika kusaka ushawishi kwa mahakama ili uamuzi wa shaurio lililopo mahakama liweze kuegemea upande fulani, bado mahakama zimeendelea kuwa imara kuhakikisha zinatenda haki kwa mujibu wa tamko la kimataifa la  haki za binadamu.

Dkt. Elifuraha Laltaika mhadhiri wa Chuo Kikuu nchini Tanzania na pia mtaalamu wa jukwaa la kudumu la watu wa asili la Umoja wa Mataifa amesema hayo akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili kuhusu wajibu wa mahakama kutoa haki.

(Sauti ya Dkt. Elifuraha Laltaika)

“Kitu kimoja kinanipa faraja kuwa pamoja na mihemuko na kupitiwa na kukosa ustaarabu kwa baadhi ya watu wakiwemo viongozi, sheria na taratibu ziko pale pale, kwamba wao wanapaswa wasikilize, wapatiwe kesi ilihusu nini, wao wanaangalia sheria wamesomea namna ya kuzitafsiri ili watoe uamuzi. Kwa hiyo kwa kiasi kikubwa sijaona mahakama zikitetereka kwa sababu ya hii mihemuko ambayo ni ya kawaida.”

Hata hivyo amezungumzia shaka na shuku akinukuu kutoka mkutano aliohudhuria karibu huko Afrika Kusini akisema..

 (Sauti ya Dkt. Elifuraha Laltaika)

“Jaji Mkuu wa Kenya alisema jambo ambalo kwa kweli sitalisahau kwa kweli ugumu wa kuamua kesi kwa siku hizi unatokana na shinikizo la maendeleo  haya ya teknolojia, kwamba jaji anaweza akashawishikika kuangalia kwenye twitter maoni ya watu yako vipi kuhusu suala hili. Kwa hiyo yeye alikuwa anatoa rai  kwa majaji wa Afrika kwamba wasiangalie sana maoni Twitter na Facebook yakoje kuhusu shauri lililoko mahakamani bali wao wawe traditionalist waangalie kwa muktadha wa sheria na ushahidi uliofikishwa mahakamani kwao.”

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.