Hayawi hayawi sasa yamekuwa, mkataba wa uhamiaji wapitishwa rasmi:

10 Disemba 2018

Baada ya majadiliano ya miezi, wiki, siku na saa, hatimaye mkataba kwa kimataifa ambao ni wa kihistoria kuhusu wahamiaji leo umepitishwa rasmi mjini Marrakesh Morocco. 

 

Shangwe na vifijo mjini Marrakesh , makataba wa kihistoria wa uhamiaji uilipopitishwa rasmi  na nchi wanachama, makampuni, asasi za kiraia, na wadau wote wa masuala ya uhamiaji kwa kauli moja. Akizungumza mara baada ya kupitishwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “mkataba huu kwa kuheshimu uhuru wa kila taifa unaanzisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa ambao ni muhimu sana wakati ambapo dunia inakabiliwa na changamoto kubwa za uhamiaji hivi sasa. Na kwamba

Mkataba huu wa uhamiaji unajikita katika masuala mawili, mosi Uhamiaji siku zote umekuwa nasi, lakini ni lazima udhibitiwe  na uwe salama na pili ni kwamba sera za kitaifa zinauwezekano wa kufanikiwa zaidi kwa ushirikiano wa kimataifa.

Amesema anaamini uhamiaji umechangia kwa kiasi kikubwa utajiri wa kimataifa, maendeleo na mafanikio, na ni kweli kwamba asilimia 80 ya wahamiaji walioko duniani hivi sasa wamefanya hivyo kwa usalama na mpangilio.Hata hivyo ameonya kwamba “Hatuwezi kusahau majanga tunayoyashuhudia kila siku jangwani, baharini, kila mahali ambako watu wanaojaribu kuwa na maisha bora wanajiweka katika mikono ya wasafirishaji haramu ambao wanakiuka haki zao za binadamu na kusababisha wengi kupoteza maisha.” Hivyo amesisitiza ni muhimu kuhakikisha haki za binadamu za wahamiaji na kuweka mazingira kwa nchi walikotoka, wanakopitia na wanakoishia kuwa mazuri na ya ushirikiano, kwa kuheshimu maslahi ya taifa lakini pia kuhakikisha haki za binadamu za watu hao. Hatuanzishi haki mpya kwa wahamiaji, Hapanatunachokianzisha ni wajibu wa kuheshimu haki za wahamiaji itakuwa si utu kuwatenga wahamiaji na tamko la haki za binadamu.

Guterres amesisitiza kuwa , anashawishika kwamba kwa ushirikiano mzuri wa kimataifa , itawezekana kuwekeza zaidi katika nchi watokako, ili kuwapa mazingira ya watu kuwa na chaguo la kubaki katika nchi zao na kuzijenga kwa matumaini ya maisha bora katika nchi zao. Na kuongeza kuwa “Naamini kwa kufanyakazi pamoja kwa moyo wa ushirikiano tunaweza kuchangia kuwa na dunia bora. Tunakuwa na fursa zaidi za jamii zenye tija katika nchi waendako kwa kuchukulia tamaduni tofauti, makabila tofauti, na dini tofauti kuwa ni faida muhimu ya uwekezaji ambao unawafanya watu kuhisi uraia wao unathaminiwa na kuhisi ni sehemu ya jamii. Naamini mkataba huu utasaidia pia utasaidia kuleta uwiano wa maendeleo katika nchi watokako, kuepuka uhamiaji wa shuruti ambao wote tunataka kuuepuka kwa gharama yoyote.

Naye mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kwa ajili ya uhamiaji wa kimataifa Louise Arbour akiunga mkono kupitishwa kwa kauali moja mktaba huo amesema

(SAUTI YA LOUISE ARBOUR)

“Hii kwa hakika ni siku nzuri, na hafla nzuri, italeta athari chanya kwa maisha ya mamilioni ya watu, wahamiaji wenyewe, watu wanaowaacha nyuma na jamii ambazo zitawahifadhi. Hili bila shaka litategemea na ari ya tukio la leo kuelekea kwenye utekelezaji wa mikakati mbalimbali ambayo mkataba huu wa kimataifa utaruhusu nchi wanachama kuiweka.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud