UNICEF yakimbizana na muda ili kuwalinda watoto 151,000 nchini Iraq.

10 Disemba 2018

Wakati mwanaharakati wa Iraq Nadia Murad ambaye pia ni manusura wa manyanyaso ya kundi la kigaidi la IS akikabidhiwa tuzo ya amani ya Nobel, shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetoa wito wa kuwaangalia maelfu ya watoto ambao wanakosa makazi ndani ya Iraq na maisha yao yako hatarini kutokana na baridi kali na mafuriko ambayo yameathiri eneo kubwa la nchi.

Akizungumzia hali hiyo mwakilishi wa UNICEF nchini Iraq, Peter Hawkins amesema, wakati dunia inaadhimisha hadithi ya ajabu Nadia Murad pamoja na kazi yake kwa ajili ya haki za bindamu, tukumbuke kuwa kuna watoto wengi nchini Iraq ambao wako katika mazingira magumu na wanahitaji msaada hata pale ambapo vurugu zitakuwa zimeisha.”

UNICEF inasema baridi nchini Iraq ni kali, mvua zinanyesha ikiambatana na theluji, na kiwango cha baridi kinaweza kushuka kiasi cha kufikia nyuzi joto sifuri katika maeneo ya kaskazini mwa nchi ambako wanaishi watu wengi kutoka jamii ya Yazidi na watoto wasio na makazi.

Halikadhalika familia nyingi ambazo zimepoteza makazi ni fukara na wanaishi katika, makazi ambayo hayana mifumo mizuri ya joto au katika kambi ambazo zina mifumo duni ya kuweza kuzuia baridi.

Taarifa ya UNICEF imesema haiwezekani kwa watu hao kumudu kununua mafuta ya kuendeshea mifumo ya kutengeneza joto na pia kununua nguo za kuzuia baridi ili kuwapa joto watoto walioko katika maeneo hayo.

Hawkins wa UNICEF ameongeza, “mafuriko mkubwa yamesababisha hali mbaya zaidi kwa watoto ambao wako hatarini zaidi kupata ugonjwa wa mwili kupoteza uwezo wa kuhimili baridi kwa kushindwa kushindwa kutengeneza joto, pia wako hatarini kupata magonjwa ya mfumo wa hewa. Hakuna mtoto anayepaswa kukutana na hatari hiyo. Kila mtoto anastahili kupata joto na afya.”

UNICEF inatoa nguo za kuzuia baridi, viatu, kofia na hata msaada wa kifedha kwa watoto takribani 161,000 katika maeneo ya Sinjar, Erbil, Dohuk, Ninawa, Anbar, Diwaniya, Basra, Salaheddin, Baghdad na Suleimaniah.

Mpango wa UNICEF unalenga kuwafikia watoto walioko hatarini zaidi wenye umri wa kuanzia miezi mitatu hadi miaka 14 wanaoishi katika kambi za waliopoteza makazi n wale waliosalia katika maeneo ambayo ni vigumu kuyafikia.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter