Changamoto za maisha zilinisukuma kuwa mchechemuzi- Rebeca Gyumi mshindi wa tuzo ya haki za binadamu 2018!

10 Disemba 2018

Mshindi wa tuzo ya mwaka huu haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Rebeca Gyumi kutoka Tanzania ambaye mwezi huu wa desemba tarehe 18 atakabidhiwa tuzo hiyo amezungumzia kile kilichomsukuma kuwa mchechemuzi wa  haki hususan za watoto wa kike kwenye taifa lake hilo la Afrika Mashariki.

Rebeca ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya ‘Msichana Initiative’ nchini Tanzania kwa miaka 8 amekuwa akihoji uhalali wa ibara ya 13 na 17 ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 nchini humo ambayo inahurusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 na 15 kwa ridhaa ya wazazi au mahakama.

Akihojiwa na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa-UNIC nchini Tanzania, Rebeca anaeleza kile kilichomvutia kutetea haki za binadamu na hususani katika kutokomeza ndoa za utotoni,“nafikiri kilichonisukuma ilikuwa ni changamoto ambazo niliziona wakati nikifanya kazi kama mtetezi wa vijana katika shirika linalowalenga vijana la FEMINA lakini ninaweza kusema hata katika makuzi yangu vilevile, niliona changamoto mbalimbali ambazo kimsingi zilikuwa zinawakwamisha wasichana wengi kupata elimu.”

Anaongeza kusema kuwa baadaye aligundua kuwa changamoto alizokuwa anaziona katika eneo lake, zilikuwa pia katika maeneo mengi mengine nchini Tanzania, “nafikiri kama msichana mara zote huwa ninajiuliza ni nini zaidi ninachoweza kufanya na namna gani naweza kuwa sauti katika pengine siyo kumaliza kabisa lakini angalau kuionesha jamii yangu ielewe kuwa ndo za utotoni si jambo zuri na uwekezaji mzuri kwa mtoto wa kike ni kuwekeza katika elimu yake.”

Rebeca Gyumi anasema ingawa alikuwa anaona matatizo mengi yanayowakumba vijana, lakini matatizo dhidi ya wasichana yalikuwa ni mengi zaidi na hasa hilo la ndoa za utotoni lilikuwa linamuumiza zaidi kwani alishiriki mikutano mingi ya kujadili namna ya kuhakikisha umri wa chini wa ndoa unakuwa miaka 18, lakini baada ya hapo hakuna hatua kubwa iliyokuwa inachukuliwa,“kwa hivyo nilijiuliza ni nini ninachoweza kufanya kama mwanasheria na kama kijana mdogo ambaye ninahisi sauti yangu ni kitu ninachoweza kuweka katika harakati hii ili kuongeza kasi ya mchakato wa kuongeza umri wa ndoa. Na hapo ndipo hata lalamiko lilipokuja ili kushinikiza umri wa kuolewa ufike miaka 18.”

Mwezi Oktoba mwaka huu wa 2018, Rebeca Gyumi alitangazwa mshindi wa tuzo ya mwaka huu ya haki za binadamu ikitanguliwa na tuzo nyingine ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa mchango wake wa kukomesha ndoa za utotoni nchini Tanzania aliyoitwaa mwezi septemba mwaka 2016.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter