Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM linawapatia hifadhi ya muda na huduma zingine za ulinzi wahamiaji na wakimbizi 2,518 ambao wamehamishwa kutoka visiwa vya Aagean vilivyoko kaskazini-mashariki mwa Ugiriki kwenda hotelini nchini humo.
Taarifa ya IOM ambayo imetolewa leo mjini Athens Ugiriki, inasema kuwa kati ya Oktoba 29 na Disemba 3 mwaka huu, hatua ambayo iliungwa mkono na Umoja wa Ulaya iliikubalia IOM kuwapatia malazi na huduma zingine wasaka hifadhi wanawake 1,086 na watoto 818 waliohamishiwa bara kutoka katika visivya vya Lesvos, Chios, Kos na Leros ambavyo vilikuwa katika hali isiyokuwa si nzuri.
Chini ya mpango wa serikali ya Ugiriki ya kupunguza mlundikano katika visiwa hivyo, mkazo unapewa kutoa usafiri na malazi kwa familia zenye watoto wenye umri mdogo, mama wajawazito, wazazi ambao hawana wasaidizi na watu binafsi wenye kiwewe.
Mkuu wa ofisi ya IOM nchini Ugiriki,Gianluca Rocco, amesema kuwa kupitia mpango tekelezi uliopewa jina la FILOXENIA, IOM inanuia kuwaondolea mateso wahamiaji na wahamiaji walioko hatarini na kuwapa hali ya maisha bora kuliko yale waliomo katika vituo vya kuwakusanya katika visiwa mbalimbali katika bahari ya Mediteranea, akiongeza kuwa wanataka kuweka makazi ya muda 6000 kuwahudumia watu hao.
Baadhi ya watu 520 wako Porto Heli huku wengine wako hotelini katika maeneo mbalimbali na wengi wao wanatoka Syria, Iraq, Afghanistan, Somalia na Palestina.
IOM kwa sasa ina hoteli 11 nchini Ugiriki ambazo zina watalaam mbalimbali ambao hutoa huduma zinazohitajika kama vile za kisaikolojia na ukalimani zikilenga kusaidia familia 493 na watu 532.