Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF ndio mkombozi na ahadi yetu kwa walionasa kwenye majanga- Guterres

Mfuko wa usaidizi wa dharura wa UN, CERF umesaidia kusambaza misaada ya dharura ya kibinadamu ikiwemo chakula kama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambako mgogoro usiomalizika umeacha wananchi bila mahitaij  ya kimsingi
MINUSCA/Nektarios Markogiannis
Mfuko wa usaidizi wa dharura wa UN, CERF umesaidia kusambaza misaada ya dharura ya kibinadamu ikiwemo chakula kama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambako mgogoro usiomalizika umeacha wananchi bila mahitaij ya kimsingi

CERF ndio mkombozi na ahadi yetu kwa walionasa kwenye majanga- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Mkutano wa mwaka wa mfuko wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi wa dharura kwa majanga yanayokumba binadamu, CERF  umefanyika leo jijini New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres amesema CERF amesihi wahisani kuchangia zaidi ili kufikia lengo la uchangiaji la dola bilioni 1 kwa mwaka lililowekwa na Baraza Kuu la umoja huo miaka miwili iliyopita.

Akihutubia wajumbe, Guterres amesema uchangiaji zaidi ili kufikia lengo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa “tunatarajia majanga zaidi ya kiasili na dharura nyingine kukukumba maeneo mbalimbali ya dunia mwaka 2019 na kuleta madhara makubwa. CERF lazima ijengewe uwezo wa kuchukua hatua haraka, na pia kusambaza mgao kwa mapema pindi tunapohisi kuwa majanga  yatatokea.

Amesema umuhimu wa CERF hii leo ni mkubwa zaidi kwa kuwa licha ya harakati za kupunguza mahitaji na kuzuia majanga, bado mfuko huo unapaswa kuhaha kusaidia walio kwenye machungu kuliko ilivyokuwa mwaka 2005 ulipoanzishwa.

Ametaja sababu za ongezeko la mahitaji kuwa ni pamoja na “ukuaji uchumi usio na manufaa na mahitaji ya kibinadamu kuzidi kuongezeka kutokana na mizozo isiyoisha na ukimbizi, ukosefu wa maendeleo, ukosefu wa usawa pamoja na mabadiliko ya tabianchi bila kusahau umaskini wa kupindukia.”

Wakazi hawa wa mji wa Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ni miongoni mwa wanufaika wa mgao wa dola milioni 9 kutoka CERF zilizopelekwa nchini  humo kukidhi mahitaji ya  kibinadamu.
OCHA/Gemma Cortes
Wakazi hawa wa mji wa Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ni miongoni mwa wanufaika wa mgao wa dola milioni 9 kutoka CERF zilizopelekwa nchini humo kukidhi mahitaji ya kibinadamu.

“CERF ni ahadi yetu ya pamoja ya kuchukua hatua kwa ufanisi katika zama hizi za ongezeko la mahitaji. Ni ujumbe wetu wa matumaini na mshikamano wa dunia wa kushikamana na watu wote walionasa kwenye majanga, na zaidi ya yote tunashikamana na wale ambao wameachwa nyuma zaidi,” amesema Guterres.

Ili kuonyesha umuhimu wa mfuko huo, Bwana Guterres amesema kutokana uwepo wake, CERF inawezesha ofisi za UN kwenye nchi husika kuanza kuratibu haraka shughuli za usaidizi pindi  janga linapotokea.

Ametoa mfano wa uhaba wa chakula uliokumba nchi nne za ukanda wa Sahel mwaka huu ambapo dola milioni 30 kutoka CERF zilikuwa na mchango mkubwa kuepusha njaa na utapiamlo huko Chad, Burkina Faso, Mauritania na Mali.

Mfuko wa dharura wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa, CERF  kwa miaka 13 ya huduma yake ya kutoa fedha kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu, umeshatoa jumla ya dola bilioni 5.5 kwa zaidi ya nchi 100 na maeneo, na hilo limewezekana kutokana na mchango kutoka nchi 126.

Awali changisho la kila mwaka kwa CERF lilikuwa dola milioni 450 lakini miaka miwili iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliongeza kiwango hadi dola bilioni 1 kutokana na ongezeko la mahitaji ya dharura duniani.