Watu zaidi ya 500 wakamatwa Papua Indonesia, UN yatiwa hofu

7 Disemba 2018

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa mataifa imesema inatiwa hofu na hatua ya kukamatwa watu zaidi ya 500 waliokuwa wakiandamana kwa amani kuadhimisha siku ya taifa Papua Magharibi.

Ofisi hiyo inasema imepokea taarifa kwamba kamatakamata hiyo imetokea tarehe mosi na pili disemba katika maeneo mbalimbali nchini Indonesia na kwamba vikosi vya usalama vilitumia vizuizi kuwazuia watu wasiandamane kwa amani mjini Jakarta, Mashariki mwa  Nusa Tenggara, Maluku Kaskazini, Merauke na pia kuvuruga ibada zilizoandaliwa na wanafunzi wa jamii za asili na kusababisha watu wengi kukamatwa na kuswekwa rumande.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Ravina Shamdasani amesema “tunaelewa kwamba kamatakamata kubwa imefanyika mjini Surabaya Java Mashariki na tumepokea habari za kutia hofu za matumizi ya nguvu kupita kiasi na ghasia kutoka kwa vikosi vya usalama wakati wa maandamano na mapigano yakazuka miongoni mwa waandamanaji huku wengine wakitoa kauli za kupinga Papua. Vikosi vya usalama pia viliendesha msako kwenye mabweni ya wanafunzi na kusababisha kukamatwa na kushikiliwa kwa nguvu takriban watu 300.”

Hata hivyo ameongeza kuwa watu hao hivi sasa wameachiliwa bila mashitaka yoyote.

Ofisi ya haki za binadamu inasema ingawa inaelea changamoto na ugumu wa hali ya Psapua kinahowasumbua ni msako unaoendeshwa dhidi ya maandamano ya Amani , ripoti za matumizi ya nguvu kupita kiasi, udhalilishaji, watu kuwekwa rumande, ikiwa ni pamoja na vitisho dhidi ya wanasheria wanaoshughulikia kesi hizo.

Ofisi hiyo imeongeza kuwa vitendo hivyo vinaonekana kama ni njia ya kubinya haki za watu za uhuru wa kushiriki, kukusanyika kwa Amani na kujieleza na vinahatarisha haki hizo za msingi kwa jamii.

Ofisi ya haki za binadamu imeitaka serikali kuchukua hatua za kushughulikia malalamiko yanayotolewa Papua na  Indonesia kutimiza wajibu wake wa kimataifa wa kutekeleza haki za msingi za binadamuna pia kutekeleza wajibu wake wa ahadi za kisiasa ilizozitoa wakati wa tathimini ya baraza la haki za binadamu.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter