Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia zaidi ya 100 wanauawa au kujeruhiwa Yemen kila wiki:UNHCR

Batola na Hussein Mohammed na watoto wao wakijiandaa kuondoka Yemen kurejea Somalia kupitia msaada wa UNHCR na IOM baada ya machafuko kuzidi nchini Yemen.
UNHCR/Shabia Mantoo
Batola na Hussein Mohammed na watoto wao wakijiandaa kuondoka Yemen kurejea Somalia kupitia msaada wa UNHCR na IOM baada ya machafuko kuzidi nchini Yemen.

Raia zaidi ya 100 wanauawa au kujeruhiwa Yemen kila wiki:UNHCR

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limetoa wito wa ulinzi zaidi kwa raia na miundombinu yao nchini Yemen baada ya tathimini yake kubaini kwamba takriban raia 1500 walijeruhiwa na wengine kuuawa kati ya Agosti na Oktoba mwaka huu, hii ikimaanisha kwamba wastani wa raia 123 waliuawa au kujeruhiwa kila wiki katika muda huo wa miezi miwili.

Shabia Mantoo msemaji wa UNHCR mjini Geneva akizungumza na waandishi wa habari hii leo amesema “kila siku mpya ya machafuko Yemen ni zahma Zaidi kwa raia ambao tayari wameshachoshwa na madhila chungunzima”.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa kwenye ripota ya ufuatiliaji wa athari za vita kwa raia (CIMP) matukio takriban 670 ya ghasia za silaha yamesababisha majeruhi na vifo vya raia 1478 katika kipindi cha miezi mitatu, huku asilimia kubwa ya waathirika ni wanawake na watoto ambapo 217 waliuawa na 268 kujeruhiwa.

Wakati huohuo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema limetoa msaada wa mgao wa chakula ambacho tayari kimeshapikwa na mgao wa kila mwezi kwa watu 50,000 ambao wameathirika na machafuko mapaya wakati kundi la kigaidi la ISIS likishika udhibiti wa eneo la Hajin wilaya ya AlbuKamal kusini Mashariki mwa jimbo la Deir Ezzor. Pia shirika hilo limesema machafuko ya wiki iliyopita Kusini mwa Idlib kulisababisha watu 15,000 kukimbia vijiji vyao na kuingia katika jimbo hilo .