Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mwananchi Kenya kuwa na umeme ifikapo 2022

Paneli za sola zikiwa dukani. Paneli hizi ni muarobaini kwenye maeneo yasiyo na umeme unaozalishwa kwa kutumia nishati nyingine.
Mohamed Nasser
Paneli za sola zikiwa dukani. Paneli hizi ni muarobaini kwenye maeneo yasiyo na umeme unaozalishwa kwa kutumia nishati nyingine.

Kila mwananchi Kenya kuwa na umeme ifikapo 2022

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Serikali ya Kenya kwa ubia na  Benki ya Dunia wamezidnua mkakati wa kuhakikisha umeme unakuwa umemfikia kila mwananchi ifikapo mwaka 2022.

Mkakati huo uitwao KNES pamoja na mambo  mengine umebainisha mbinu rahisi za kusambaza umeme kwenye kaya na maeneo ya biashara kwa gharama nafuu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia, mkakati huo umezingatia ukweli kwamba gharama nafuu ya umeme inawezekana kwa kuwa na vyanzo vya umeme visivyounganishwa moja kwa moja na gridi ya taifa pamoja na kushirikisha sekta binafsi.

Mathalani  vituo vidogo vya umeme na vyanzo vya nishati ya umeme inayotokana na jua.

 Akizungumzia hatua hii Waziri wa nishati wa Kenya Charles Keter amesema kumekuwepo na mafanikio makubwa ya kusambaza umeme katika miaka ya karibuni na kufikia asilimia 75 ya wananchi.

“Hata hivyo kulikuwa na umuhimu wa kuwa na mkakati wa kitaifa wa kusambaza umeme ili kushughulikia changamoto za kuhakikisha umeme unapatikana nchini kote kwa gharama nafuu,” amesema Waziri Keter.

BENKI YA DUNIA YAAZIMIA KUFANIKISHA KNES

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Kenya Felipe Jaramillo amesema benki hiyo imeazimia kusaidia Kenya kusambaza nishati salama na ya kisasa kwa wananchi wake wote kwa gharama nafuu.

 “Hivi sasa Benki ya Dunia inafadhili mradi wa kuboresha huduma ya umeme  nchini Kenya,  KEMP na ile ya mradi wa umeme wa nishati ya jua au sola, KOSAP. KEMP inalenga kaya mpa 235,000 ilhali KOSAP kaya mpya milioni 1.3,” amesema Bwana Jaramillo.

Takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu bilioni moja duniani kote hawana umeme, na nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na zile za kusini mwa Asia ndio zinaongoza kwa kukosa huduma hiyo muhimu ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kenya inasema mkakati huo wa kusambaza umeme nchini kote ni muhimu ili kufanikisha dira yake ya maendeleo ya mwaka 2030 sambamba na ajenda zake kuu nne ambazo ni makazi nafuu, viwanda, uhakika wa chakula na huduma ya afya kwa wote.

Mkakati wa kusambaza umeme nchini Kenya uliandaliwa kwa usaidizi kutoka ESMAP ambao ni program ya ubia kati ya Benki ya Dunia na wadau 18 wa maendeleo ambao wanasaidia nchi za kipato cha chini na kati kupunguza umaskini na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa mbinu endelevu za mazingira.