Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya Yemen na wahouthi wote wanataka mapigano Yemen yakome- Griffiths

Mkutano na waandishi wa habari Rimbo, Sweden. Wa pili kutoka kulia ni Martin Griffiths, mjumbe maalum wa UN kwa Yemen na kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Margot Walstrom
Screen shot- video
Mkutano na waandishi wa habari Rimbo, Sweden. Wa pili kutoka kulia ni Martin Griffiths, mjumbe maalum wa UN kwa Yemen na kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Margot Walstrom

Serikali ya Yemen na wahouthi wote wanataka mapigano Yemen yakome- Griffiths

Amani na Usalama

Siku ya kwanza ya mashauriano kati ya pande kinzani nchini Yemen ikikamilika huko Rimbo, nchini Sweden, Umoja wa Mataifa umetaja mambo matatu ambayo unatamani yatokane na mkutano huo wa kwanza kabisa kati ya pande hizo baada ya miaka miwili. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Rimbo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Martin Griffiths ametaja mambo hayo kuwa ni mosi kujadili mfumo wa mazungumzo unaoweza kufanikisha suluhu, akisema kuwa kinachofanyika sasa ni mashauriano si majadiliano.

“Pili kuna harakati za kujenga imani ili kusaidia kupunguza machungu ya wayemeni na kujenga imani ikiwemo kuachia wafungwa, makubaliano ambayo yametiwa saini na pande zote, na pia suala la kufungua uwanja wa ndege wa Sana’a na jinsi pande zote zinaweza kuchangia kwenye mipango ya kiuchumi. Tatu ni kupunguza ghasia Yemen.”

Bwana Griffiths akafafanua ujumbe kutoka viongozi wa pande zote za mazungumzo akisema..

“Wameniambia kuwa kile tunachotaka kinafanyika Sweden na kile ambacho wayemen wanataka kuona kinafanyika Sweden ni kupungua kwa ghasia . Kwa hiyo mabadiliko ya dhahiri kwa maisha ya watu kama ambavyo ingalikuwa kwa mtu yeyote hata sisi mwenye familia katika mazingira kama hayo.”

KINACHOFANYIKA SWEDEN NI KWA MASLAHI YA WASIOPO KWENYE MEZA YA MAZUNGUMZO

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa amesema kwa mazingira ya sasa ya Yemen kuna umuhimu wa kusonga mbele haraka kusaka suluhu kwa kuzingatia pia jamii ya kimataifa ikiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, imeungana pamoja akisisitiza kuwa “tunafanya hiki si kwa maslahi ya watu waliomo kwenye chumba hiki bali kwa maslahi ya wale wasiomo humu ndani. Tunataka kunufaisha wayemen.”

Mkutano huo wa mashauriano unahudhuriwa pia na makundi mawili ya washauri ambayo ni wawakilishi wa wanawake wa Yemen pamoja na wabobezi wa masuala ya siasa na utawala huko Yemen.

Sweden ambayo ndio mwenyeji wa mazungumzo hayo, kupitia Waziri wake wa mambo ya nje, Margot Wallström akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari ameshukuru pande zote kwa utayari wao wa kukutana na kujadili mustakhbali wa Yemen.