Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Yemen zikikutana Sweden, sauti zapazwa ili ziweke mbele maslahi ya watoto

Vijana wa Yemen wakiwa wamekalia magodoro waliyopewa na UNHCR Sirwan, Yemen. Zaidi ya milioni mbili wamesambatishwa na mapigano ya Yemen.
MDF/M. Hudair
Vijana wa Yemen wakiwa wamekalia magodoro waliyopewa na UNHCR Sirwan, Yemen. Zaidi ya milioni mbili wamesambatishwa na mapigano ya Yemen.

Pande kinzani Yemen zikikutana Sweden, sauti zapazwa ili ziweke mbele maslahi ya watoto

Amani na Usalama

Wawakilishi wa serikali ya Yemen na wale wa kundi la Houthi wakikutana kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili kwa mazungumzo nchini Sweden hii leo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Martin Griffiths amesema fursa hiyo inaleta matumaini ya kuanza tena kwa mchakato wa amani nchini humo.

Bwana Griffiths amesema hayo kupitia tahariri yake iliyochapishwa kwenye gazeti la New York Times, wakati huu ambapo hali ya amani huko Yemen si shwari, watoto wakiwa hoi bin taaban, miundombinu ya kijamii ikiwa imesambaratishwa na jamii haina mwelekeo.

Mathalani, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Geert Cappelaere ambaye ametembelea Yemen, hali ya maisha kwa mamilioni ya watoto inakatisha tamaa.

Ameshuhudia maisha ya kihohehahe miongoni mwa watoto na familia zao, watoto ambao hata hivyo wakati akizungumza nao wengine walionekana hoi ilhali wengine bado wana hamu ya kucheza akifafanua zaidi kuhusu mtoto Abir...“Mazingira ambamo nimemkuta nayo Abir hapa na watoto wengine yanasikitisha. Hakuna kabisa chakula. Shukrani kwa UNICEF kwa sababu angalau wanapata maji kila siku lakini hakuna huduma za kujisafi. Haishangazi kuwa katika maeneo kama haya tatizo la kipindupindu au magonjwa mengine ya kuhara yameshamiri hasa kwa watoto.”

 Ameongeza kuwa “machungu wanayopitia watoto yamesababishwa na binadamu. Zaidi ya watoto 2,700 wametumikishwa kwenye mapigano yanayoendelea, zaidi y a 6,700 wameuawa au wamejeruhiwa ilihali takribani watoto milioni 1.5 wamefurushwa kwenye makazi yao.”

Halikadhalika amegusia pia hali ya chakula akisema watoto milioni 7 nchini Yemen kila siku wanalala bila mlo ilhali watoto 400,000 wanakabiliwa na unyafuzi.

Ni kwa kuzingatia hali duni ya watoto na kutokuwepo kwa nuru yoyote hivi sasa, Bwana Cappelaere amesihi wawakilishi wanaokutana nchini Sweden na wale wote wenye ushawishi juu yao kupatia kipaumbele watoto na mahitaji  yao badala ya kujali ajenda zao za kisiasa, kijeshi au kifedha.

“Mustakabali wa watoto wa Yemen uko mikononi mwenu,” amesema Bwana Cappelaere.

Kwa mujibu wa mjumbe maalum wa UN kwa Yemen, mwishoni mwa awamu hii hii ya mazungumzo huko Sweden, pande mbili hizo zinatarajiwa kuwa zimekubaliana juu ya muundo mwa mkataba wa kina ambao utaonesha mpango mzima kuelekea kwenye amani.