Elimu si karatasi, ni kuelimika

6 Disemba 2018

Makadirio ya shirika la kazi duniani ILO yaliyotolewa mwaka uliopita wa 2017, yalionesha kuwa upatikanaji wa ajira kwa vijana utaendelea kuzorota kwa  mwaka huu wa 2018 ambapo vijana milioni 71.1 sawa na asilimia 13.1 ya vijana wote kote duniani hawatakuwa na ajira. Miongoni mwa vijana hao wasiokuwa na fursa ya kupata ajira rasmi ni Situmai Simba msichana mwenye umri wa miaka 24 aliyeanzisha biashara ya uji, ambao kutokana na ubunifu, anamudu kupambana na hali hii ya ukosefu wa ajira kwa kubuni miradi mipya inayowaajiri wao na wenzao.

Situmai, akiwa na shahada ya kwanza aliyoipata katika Chuo cha Usimamizi wa fedha, IFM, nchini Tanzania, ameanzisha biashara ya kuuza uji mjini Dar es Salaam na katika mazungumzo na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa,UNIC nchini Tanzania Situmai anaanza kwa kueleza aina za uji anaouza,

Nauza uji wa aina mbalimbali kwa mfano uji wa mchele, wa ulezi, mtama, ngano,tende na nauza kwa shilingi elfu moja za Tanzania (takribani nusu dola ya dola za kimarekani) mtu anaweza akabeba akaenda nao ofisini. Nimetimiza mwaka, nimeanguka mara mbili lakini nimepata fundisho kubwa lakini nina imani nitazidi kusimama zaidi. Sasa hivi nimefungua tawi jipya katika Hospitali ya Muhimbili kwa hivyo kwa sasa nina matawi mawili Posta na Muhimbili.”

Akijibu kuhusu namna ambavyo biashara yake imepokelewa katika jamii, Situmai anasema anashukuru sana kwani tayari ndani ya mwaka mmoja ameshapata tuzo mbili moja ikiwa yenye jina la Malkia wa nguvu na tuzo nyingine ikiitwa Nguvu ya uthubutu na anaamini atafanya vizuri zaidi.

Situmai anasema mwanzoni alipoanza biashara hii alikuwa anaamka alfajiri ya saa kumi, anapika uji, kuupakia na kuupeleka katika eneo la biashara, lakini sasa mzigo umekuwa mkubwa kwa hivyo amewaajiri vijana wengine watano kumsaidia.

“Kuna mpishi ambaye anapika kisha uji unaenda kwenye vituo, na huko kwenye vituo kuna watu ambao wanaangalia mauzo na kusambaza kwenye ofisi zilizo karibu na vituo hivyo” anasema Situmai.

Malengo yake ni kufikia kiwango cha kuweza kusambaza bidhaa zake za uji kote duniani. Anasema anawaza kutengeneza uji utakaohifadhiwa kwa namna ambayo mteja akinunua kokote duniani anaweza tu kuchanganya na maji ya moto na uji ukawa tayari kunywewa.

“Ujumbe ambao ninataka kuwaachia vijana ni tusichague kazi. Umesoma una shahada usichague kazi kwa kuamini hailingani na elimu yako”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter