Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kubakwa kwa wanawake na wasichana Sudan Kusini, UN na AU watoa taarifa ya kuchukizwa na ukatili huo wa kingono

Ujumbe wa ngazi ya juu wa UN na AU huko Sudan Kusini ambapo wakati huo wanawake walikuwa na matumaini sambamba na hofu.
UNMISS/Isaac Billy
Ujumbe wa ngazi ya juu wa UN na AU huko Sudan Kusini ambapo wakati huo wanawake walikuwa na matumaini sambamba na hofu.

Kubakwa kwa wanawake na wasichana Sudan Kusini, UN na AU watoa taarifa ya kuchukizwa na ukatili huo wa kingono

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU wametoa taarifa ya pamoja ya maelezo yao juu ya kuchukizwa na na visa vya ukatili wa kingono, ikiwemo kubakwa, vilivyotekelezwa dhidi ya wanawake na wasichana takriban 150 karibu na mji wa Bentiu nchini Sudan Kusini mwishoni mwa mwezi uliopita.

Taarifa hiyo ya pamoja imetolewa na mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean Pierre Lacroix, kamishna wa amani na usalama wa muungano wa Afrika, AU Balozi Smaїl Chergui na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na maswala ya wanawake, UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka.

 

Wakirejelea ziara yao ya pamoja nchini Sudan Kusini na Bentiu miezi miwili iliyopita, watatu hao wameangazia kuendelea kwa ukatili unaoelekezwa dhidi ya wasichana na wanawake na ukosefu wa uwajibikaji.

 

Wamesema wakati wa ziara yao, walikutana na wanawake ambao walikuwa na matumaini kuhusu makubaliano mapya ya kutatua mzozo nchini Sudan Kusini mwezi Septemba mwaka huu lakini wakihofia amani dhaifu na usalama katika jamii. Wakitaja ukatili huo kama tabia isiyokubalika na ambayo inahitaji kutokomezwa mara moja.

Mtoto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya muda ya kulinda raia huko Bentiu nchini Sudan Kusini.
UNICEF/Holt (file)
Mtoto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya muda ya kulinda raia huko Bentiu nchini Sudan Kusini.

 

Kwa pamoja wamerejelea wito wao kwa mamlaka za serikali kushughulikia ukatili wa kingono.

 

Ikizingatiwa kuwa mashambulizi hayo yametokea katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali, wametolea wito Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na viongozi kuweka kwa haraka juhudi za kuzuia visa kama hivyo ikiwa kwa kuchukua hatua za hivi sasa za kisheria na za uwajibishaji.

 

Wameomba pande husika kwenye mzozo kutekeleza wajibu wao katika kushughulikia matukio ya ukatili wa kingono na kurejesha hadhi ya wanawake na watoto nchini Sudan Kusini na kuwawajibisha washukiwa.

 

Umoja wa Mataifa na AU umeelezea utayari wake kusaidia pande husika katika kutafuta suluhu ya kisiasa kwa mzozo kupitia makubaliano yaliyotiwa saini, pamoja na kuchagiza kuhusu usalamwa wa wanawake na watoto na ufikiaji wa huduma muhimu na sheria.