Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wachunguzi wa haki za binadamu wamiminika Bentiu Sudan Kusini kuchuguza visa vya ubakaji.

Mlinda amani wa UNMISS akishika doria katika barabra karibu na Bentiu, jimbo la Unity, Sudan Kusini.
UNMISS Photo
Mlinda amani wa UNMISS akishika doria katika barabra karibu na Bentiu, jimbo la Unity, Sudan Kusini.

Wachunguzi wa haki za binadamu wamiminika Bentiu Sudan Kusini kuchuguza visa vya ubakaji.

Wanawake

Wachunguzi wa masuala ya haki za binadamu wanamiminika huko Bentiu  nchini Sudan Kusini kuchunguza madai ya visa vya kubakwa kwa wanawake na wasichana 150 kwa siku 10 mwishoni mwa mwezi uliopita.

Miongoni mwao ni Andrea Cullinan kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA, ambaye pia ni  mratibu wa kitaifa wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, yanayohusika na  kuzuia ukatili wa kijinsia nchini humo.

Bi. Cullinan amesema hata kama mtu mmoja amebakwa bado hicho kitendo hakifai na kwamba “ubakaji wowote ule hata uwe wa mtu mmoja, 10 au 100, tunamhudumia kila mwanamke kwa utu anaostahili.”

Ndege ambayo alisafiria Cullinan kuelekea Bentiu ilikuwa imechukua pia jopo lingine la wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ambao lengo lao ni kuongeza nguvu ya wale waliomo nchini Sudan Kusini.

Akizungumzia ujio wa msururu wa wachunguzi, mkurugenzi wa haki za binadamu wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS, Eugene Nindorera amesema, “kwa sababu ya kiwango cha tuhuma na idadi ya wanawake na wasichana waliobakwa, tuliona ni vyema kuwa na watu wengi zaidi kufanya uchunguzi.”

UNMISS ina jukumu la kufuatilia, kuchunguza, kuthibitisha na kutoa taarifa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji, sambamba na ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu ikiwemo mizozo inayohusiana na ukatili wa kingono.

Ni kwa kuzingatia madai hayo ya ubakaji wakati huu ambapo idadi ya visa ilipungua kutokana na makubaliano ya amani ndio maana Bwana Nindorera amesema, “inasikitisha sana kuona kuwa hili linatokea sasa na nadhani tunapaswa kuchukua hatua haraka.”

Taarifa kuhusu ubakaji zilitolewa na shirika la misaada la madaktari wasio na mipaka MSF ambalo lilitangaza tarehe 30 mwezi uliopita kuwa limepokea katika zahanati yao ya Bentiu wanawake na wasichana ambao walidai kubakwa.

Idadi yao inakisiwa kufikia 150, lakini baadhi ya viongozi wa sehemu hiyo wanapinga madai hayo.