Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kigeugeu kwenye mkataba wa kimataifa wa uhamiaji ni taswira mbaya kwa nchi husika:Abour

Wasaka hifadhi wakiokolewa na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea
Frontex/Francesco Malavolta
Wasaka hifadhi wakiokolewa na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea

Kigeugeu kwenye mkataba wa kimataifa wa uhamiaji ni taswira mbaya kwa nchi husika:Abour

Wahamiaji na Wakimbizi

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya uhamiaji wa kimataifa  Louise Abour amesema dhamira iliyowekwa bayana na nchi kadhaa ikiwemo Hungary, Poland , Jamhuri ya Czech na Australia ya kujiengua kwenye mkataba wa kimataifa wa wahamiaji inaonyesha picha mbaya kwao na ina athari kubwa katika ari ya ushirikiano wa kimataifa . 

Akizungumza katika mahojiano maalumu na UN News Bi. Abour ametaja kwamba mkataba huo uliafikiwa baada ya majadiliano ya kina yakihusisha nchi zote wanachama isipokuwa Marekani , majadiliano yaliyodumu kwa miezi kadhaa ambapo kila nchi iliwasilisha dhamira yake na kuafikiana na wengine , na ameongeza kuwa hilo ndilo linalosikitisha zaidi kuona kwamba nchi zinageuka kinyonga na kubadili maamuzi yake ya kutia saini mkataba huo mara tu baada ya kuafikiana pande zote zilizoshiriki.

Hivi karibuni duru za habari zimesema waziri mkuu wa Slovakia alikuwa kiongozi wa karibuni wa kitaifa kutangaza kujiondoa kwenye uungaji mkono wa mkataba huo. Hata hivyo Bi. Abour amesema mataifa mengi bado yameridhia mkakati huo kuhusu wahamiaji, ambao ni mkataba wa ushirikiano usio na athari za kisheria na wenye lengo la kuweka mikakati ya kufanya uhamiaji wa kimataifa kuwa salama, wa mpangilio na wa kawaida.

Mkataba huo unalenga kushughulikia shuku za nchi zinazotia saini na wakati huohuo ukichagiza uhuru wa mataifa, na kutambua madhila yanayowakabili wahamiaji. Amesisitiza kuwa mara utakapotekelezwa utatoa fursa kwa nchi wanachama na wahamiaji kushamiri.

Hakuna shaka kwamba tutashuhudia mavuno ya faida za wahamiaji na la msingi zaidi itapunguza baadhi ya hulka hasi kama za uhamiaji wa kiholela na watu kuhamia katika njia ambazo ni za vurugu na za hatari.”

Katika faida za kimaendeleo amesema“Tutashuhudia mabadiliko makubwa katika upande wa maendeleo, upande wa masuala ya kibinadamu na nyanja zote za faida za kiuchumi ambazo zinaweza kuletwa na wahamiaji, endapo mkataba huo utasimamiwa vyema  na kwa njia ya ushirikiano.”

Akizungumzia mtazamo mbaya ambao mara nyingi huusishwa na wahamiaji Bi. Abour amesema , sera za serikali zinapashwa kuongozwa na takwimu na kulingana na hali halisi kwani.

“Kuna nchi nyingi duniani hii leo ambazo zingependa kuingiza toka nje sehemu kubwa ya nguvu kazi yake , mazingira yanaonyesha kwamba endapo wanataka kushikilia viwango vyao vya kiuchumi vya sasa au hata kukua zaidi kiuchumi, watahitaji kupata wageni walio na ujuzi ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira katika nchi zao.”

Amesema, kuwa na utamaduni wa kibaguzi katika hali hiyo itakuwa ni hasara kwao.   Mkataba huo wa kimataifa kuhusu wahamiaji unatarajiwa kupitishwa rasmi kwenye mkutano utakaofanyika mjini Marrakeshi Morocco mwezi Desemba mwaka huu ambako Bi. Abour anasema anatarajia nchi wanachama kuelezea nia ya kutekeleza vipengee ambavyo ni muhimu kwao, kuweka bayana dhamira zao, kubadilishana mawazo bunifu na kuunda ushirika Zaidi kuhusu suala la uhamiaji.

Mkutano huo pia utashuhudia uzinduzi wa Mtandao wa uhamiaji utakaofanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Chombo hicho kinaratibiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM), ambacho kitasimamia utekelezaji wa mkataba wa kiamataifa wa uhamiaji na kuhusiha mashirika yote ya Umoja wa Mataifa ambayo yanajumuisha Nyanja ya uhamiaji katika majukumu yake.