Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya kisasi kwa mashahidi wa ukiukwaji wa haki vinasikitisha- Farha

Majengo ambayo hayajakamilika mjini Cairo Misri.
World Bank/Kim Eun Yeul
Majengo ambayo hayajakamilika mjini Cairo Misri.

Visa vya kisasi kwa mashahidi wa ukiukwaji wa haki vinasikitisha- Farha

Haki za binadamu

Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za kuwa na makazi amelaani vikali hatua ya kuwaondoa kwa nguvu watu, kubomoa nyumba za watu, kuwamata kiholela, kuwakandamiza na ulipizaji kisasi dhidi ya watu aliokutana nao katika ziara yake ya uchunguzi nchini Misri kuanzia Septemba 24 hadi Oktoba 3 mwaka huu wa 2018.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, mjumbe huyo Leilani Farha, anasema kuwa Misri imeshindwa kutekeleza  hakikisho alilopewa kuwa hakuna mtu atakayedhalilishwa au kutendewa visa vya ulipizaji kisasi kwa kukutana naye ama kutoa taarifa kwake au kwa ujumbe wake katika ziara yao nchini humo.
 
Bi. Farha ameelezea kusikitishwa kwake na taarifa kuwa familia kadhaa  kutoka jamii mbili alizotembelea  zimelazimishwa kuondoka kwa lazima ambayo kinyume na sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu. Pia majengo kadhaa ya ghorofa yamevunjwa, huku vyombo vyao vikitupwa na wakazi kuachwa bila makazi.
 
Kwa upande wao wataalam maalum wameelezea wasiwasi wao kuhusu serikali ya Misri kuweka vizuizi dhidi ya Bi Farha zilizokwamisha uwezo wake wa kuwasiliana na kuzungumza bila uoga wowote na mashahidi na wale ambao haki zao zinakandamizwa nchini humo.
 
Bi Farha kwa upande wake ameelezea kukatishwa tamaa kutokana na kushindwa  kufika katika kisiwa cha Warrag ambako kunashuhudiwa mvutano kati ya wakazi na watawala kuhusu bomobomoa ya nyumba za wakazi hao.
 
Naye mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu watetezi wa haki za binadamu, Michel Forst, amesema kuwa watetezi wa haki za binadamu na mawakili wanaoshughulikia haki za nyumba nao wanasema wanaandamwa na kupigwa picha na watu wasiojulikana, na wengine wamepokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana ama kuambiwa kufika kituo cha polisi kuhojiwa. Halikadhalika wakili mmoja ambaye alikutana na Farha katika ziara ya kikazi alipigwa marufuku ya kusafiri.
 
Baraza la haki za binadamu limekariri, katika mapendekezo yake kadhaa kuwa, kila mtu ana haki ya kupata mawasiliano na mfumo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa bila kizuizi chochote na hivyo kuzihimiza serikali kujizuia dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na kisasi.
 
Hivyo Misri imetolewa wito kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atakayedhulumiwa kutokana na ziara ya ujumbe maalum nchini Misri na pia kuwapa makazi mengine ama kuwalipa fidia  wale wote waliofurushwa kuambatana na sheria za kimataifa za haki za binadamu.