Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchumi na ujumuishwashi wa vijana vitapiga jeki mabadiliko ya tabia nchi:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiuhutubia mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi COP24 unaoendelea mjini Katowice , Poland 2018 . Pembeni yake ni Luis Alfonso de Alba mwakilishi wake maalumu wa mkutano wa  mwaka 2019. Mwanzoni
UNFCC Secretariat/James Dowson
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiuhutubia mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi COP24 unaoendelea mjini Katowice , Poland 2018 . Pembeni yake ni Luis Alfonso de Alba mwakilishi wake maalumu wa mkutano wa mwaka 2019. Mwanzoni kushoto ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu, Robert Orr

Uchumi na ujumuishwashi wa vijana vitapiga jeki mabadiliko ya tabia nchi:Guterres

Tabianchi na mazingira

Ari, mabadiliko ya kiuchumi na ujumuishwaji wa raia ni mambo matatu muhimu yatakayomulikwa katika mkutano ujao wa 2019 wa mabadiliko ya tabia nchi .

Hayo yameelezwa leo kwenye mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi COP24 unaoendelea mjini Katowice , Poland ukisaka muongozo wa kimataifa kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Akizungumza hii leo mbele ya waandishi wa habari na wadau kwenye mkutano huo ulioandaliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi UNFCCC, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasilisha maono yake ya   mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi wa 2019 .

“Mkutano huo utajikita katika kuhakikisha mambo muhimu matatu: kuamsha ari ya kweli, kuchukua hatua halisi za mabadiliko katika uchumi na ushirikishwaji wa raia na uhamasishaji wa vijana,”

Nia ya mkutano huo uliopangwa kufanyika tarehe 23 Septemba 2019 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani ni kuchagiza msaada na uungwaji mkono wa hatua za mabadiliko ya tabia nchi katika ngazi ya kisiasa amesema Guterres na kuongeza kuwa “tutafanya mkutano huo wakati wa wiki ya vikao vya ngazi ya juu vya Baraza Kuu ili kuhakikisha tuna wakuu wengi wa nchi na viongozi wa serikali watakaohudhuria kadri iwezekanavyo watakaohudhuria.”

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kawaida huhudhuriwa na takribani viongozi  na wakuu wa nchi 130 kujadili na kuweka ajenda za kimataifa kwa mwaka huo. Guterres amewaeleza washiriki kwamba, “Matokeo ya mkutano huo yatakuwa matokeo yenu “ Amezialika serikali zote , sekta za biashara, taasisi za fedha, sekta za umma na binafsi pia asasi za kiraia kushiriki katika mchakato wa maandalizi.

Alipoulizwa endapo Umoja wa Mataifa una mpango wa kufanya mazungumzo  na nchi wazalishaji wa nishati ikiwemo mafuta, gesi na makaa ya mawe amesema mazungumzo tayari yameshaanza na ingawa  wakati mwingine kuna changamoto katika sekta hiyo na ni vigumu , lakini sekta hizo zimeendelea kutambua haja ya kuhamia kwenye suluhu ya nishati mbadala.

Mkutano huo wa 2019 pia utaangazia masuala sita : mabadiliko kuelekea nishati mbadala, ufadhili wa hatua za mabadiliko ya tabia nchi, na gharama za hewa ya ukaa, kupunguza uchafuzi utokanao na gesi ya viwandani, kutumia maliasili kama suluhu, kuwa na miji endelevu, hatua kuanzia mashinani na mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Na ili kuongoza njia ya kuelekea kwenye mkutano huo mwezi uliopita Katibu Mkuu alimteua Luis Alfonso de Alba kama mwakilishi wake maalumu wa mkutano huo. Akihudhuria pia mkutano wa COP24, mwakilishi huyo amesema kwamba moja ya vipaumbele vyake katika miezi ijayo ni kushirikiana kwa karibu na kila mdau wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi ili kuwahamasisha. “lengo sio kujadiliana matokeo bali ni uhamasishaji wa ushiriki wa ngazi ya juu , kuchagua nini kitakachokwenda kwenye mkutano kwa mantiki ya hamasa na ubunifu na kisha kuwa na mukhtasari wa majadiliano wakati wa mkutano wenyewe.”

Na katika kufungua pazia la mkutano huo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na mkutano maalum mwezi Machi 2019.