Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Migogoro na mabadiliko ya tabia nchi vyaendeleza zahma ya kibinadamu duniani:OCHA Ripoti

Baadhi ya nyumba za  mtaa wa Shejaiya Gaza zilibomolewa katika mgogoro.
UNICEF/El Baba
Baadhi ya nyumba za mtaa wa Shejaiya Gaza zilibomolewa katika mgogoro.

Migogoro na mabadiliko ya tabia nchi vyaendeleza zahma ya kibinadamu duniani:OCHA Ripoti

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, leo limezindiua ripoti ya ya takwimu na mwenendo wa hali ya binadamu duniani kwa mwaka 2018 (WHDT) ikijikita katika takwimu za kipindi cha miaka mitano.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa mjini Geneva Uswisi imetolewa sanjari na tathimini ya mtazamo wa kibinadamu kwa mwaka 2019 ambao unatathmini  mahitaji ya kibinadamu na jinsi ya kukabiliana nayo kwa kuangalia ushahidi. Ripoti hiyo (WHDT) ambayo hutolewa kila mwaka huwasilisha takwimu na tathmini kuanzia ngazi ya taifa hadi kimataifa kuhusu migogoro ya kibinadamu na misaada.

Mbali ya kutoa takwimu ripoti pia inaonyesha ni jinsi gani mtazamo wa dunia unabadilika na fursa zilizopo za kuboresha uchukuaji wa hatua za kibinadamu.

Mzizi wa ripoti hiyo unashikiliwa na ajenda ya kiutu kwa kuzingatia majukumu matano muhimu ya kutekeleza na kufanikisha masuala ya kiutu.

Idadi ya migogoro:

Katika muongo uliopita muda na idadi ya migogoro ya kibinadamu imeongezeka. Kati ya mwaka 20005 na 2017, idadi ya migogoro inayopokea misaada ya kimataifa imeongezeka karibu mara mbili kutoka 16 hadi 30 , huku muda ambao migogoro hiyo inadumu na maombi ya kukabiliana nayo vikienda sanjari.

Watoto wakiwa katika kambi ya Rukban nchini Syria. Ni wakimbizi wa ndani mwa nchi.
WFP
Watoto wakiwa katika kambi ya Rukban nchini Syria. Ni wakimbizi wa ndani mwa nchi.

 

Watu kutawanywa:

Takriban watu milioni 16.2 walitawanywa upya na machafuko na vita mwaka 2017 pekee, hii ikiwa ni sawa na watu 44,000 wakilazimishwa kukimbia makwao kila siku watu wengine milioni 18.8 walilazimika kufungasha virago kutokana na majanga ya asili na hivi sasa duniani kote kuna watu wapatao milioni 70 waliotawanywa wengi ndani ya mipaka yao.

Syria ikiongoza  ikiwa na wakimbizi wa ndani milioni 6.8 ikifuatiwa na Colombia milioni 6.5 , Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo, DRC milioni 4.5, Sudan milioni 2.1 na Iraq milioni 2.

Kwa mujibu wa ripoti majanga huathiri watu milioni 350 kila mwaka na kusababisha hasara ya mabilioni ya dola . Mabadiliko ya tabia nchi yanaelezwa kuweza kuongeza idadi ya wakimbizi wa ndani hadi kufikia milioni 140 ifikapo 2050. Na bila suluhu ya kudumu kwa migogoro ya muda mrefu mwenendo huu unatarajiwa kuendelea.

 

 Watoto zaidi ya 43,000 walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati huenda wakafariki mwaka 2019 kutokana na utapiamlo uliokithiri.UNICEF
UNICEF/Ashley Gilbertson
Watoto zaidi ya 43,000 walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati huenda wakafariki mwaka 2019 kutokana na utapiamlo uliokithiri.UNICEF

 

Njaa na utapiamlo:

Baada ya kupungua kwa miaka mingi idadi ya watu wenye lishe duni inaongezeka kwa sababu ya migogoro na mabadiliko ya tabianchi, vita vinafurusha watu kutoka katika maeneo yao ya kilimo  na kuvuruga masoko ya chakula na mifumo ya usafiri, inalazimu be iza vyakula kupanda huku mabadiliko ya tabia nchi yakichochea mzunguko wa ukame na mafuriko.

Ripoti inasema mwaka 2017 watu milioni 821 walikabiliwa na lishe duni ukilinganisha na watu milioni 804 mwaka 2016 . Na katika nchi 51 watu milioni 124 hawakuwa na uhakika wa chakula ikiwa ni ongezeko la asilimia 16 ukilinganisha na mwaka 2016 na nchi zilizoathirika zaidi ni Nigeria, Somalia, Sudan kusini na Yemen. Watoto milioni 50.5 wa chini ya umri wa miaka 5 walikumbwa na utapiamlo uliokithiri mwaka 2017 na kuweka rehani maisha yao. Asilimia 80 ya watoto waliodumaa kutokana na utapiamlo mkali wanaishi katika nchi zenye vita na leo hii kuna tisho kubwa la baa la njaa nchini Yemen. Watu bilioni 2.1 hawakuwa na maji salama ya kunywa na wengine karibu bilioni 2 wanaishi kwenye maeneo yaliyo na adha kubwa ya maji.

 

Nyumba zikiwa zimetwamishwa na maji huko nchini Nigeria kutokanana mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizoanza kunyesha tangu katikati ya mwezi Julai mwaka 2018
OCHA/UNDAC
Nyumba zikiwa zimetwamishwa na maji huko nchini Nigeria kutokanana mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizoanza kunyesha tangu katikati ya mwezi Julai mwaka 2018

Wanawake na  wasichana:

Uzalishaji wa silaha, kutawanywa na kuporomoka kwa utawala wa sheria kutokana na majanga na vita kumechochea kuongezeka kwa tatizo la kutokuwepo usawa wa kijinsia na kuzagaa kwa ukatili wa kingono . Mwanamke mkimbizi mmoja kati ya watano amepitia ukatili wa kingono na idadi kamili inaweza kuwa kubwa zaidi. Wasichana wako kwenye hatari ya kutohudhuria shule mara 2.5 zaidi ya wavulana katika migogoro. Na pia ndio walio katika hatari ya kukosa elimu kutokana na majanga kama ukame kwa sababu ya kutumwa kwenda kusaka maji na kuhudumia familia.

Ripoti inasema asilimia 60 ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya wakati wa kujifungua vinatokea katika mazingira ya vita , wakati watu wametawanywa au kwenye majanga ya asili kwa sababu wanawake na wasichana vigori hawawezi kupata huduma muhimu za afya wanazohitaji.

 

Vijana wa kiume wakiwa wamesimama katika jengo lililobomolewa sehemu za Saada,Yemen
WFP/Jonathan Dumont
Vijana wa kiume wakiwa wamesimama katika jengo lililobomolewa sehemu za Saada,Yemen

Mashambulizi kwenye vituo vya afya na shule:

Mashambulizi kwenye vituo vya afya na dhidi ya wahudumu wa afya katika maeneo yenye vita yanaendelea. Kwa mwaka 2017 wahudumu wa afya walikabiliwa na mashambulizi zaidi ya 700 na mengine mengi ambayo hayakuripotiwa . Mashambilizi dhidi ya wahudumu wa afya na vituo vya afya yana athari kubwa kwa watu kupata huduma muhimu na wengine hupoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma hizo.

Shule na watoa elimu nao wameendelea kuwa mashakani wakilengwa katika machafuko. Mwaka 2017 kumekuwa na ongezeko la asilimia 24 ya mashambulizi dhidi ya shule na wato elimu ikilinganishwa na mwaka 2016. Na jumla ya watoto milioni 263 kote duniani hawakuandikishwa shule za msingi au sekondari .