Akiwa COP24 Guterres ataja mambo manne muhimu

3 Disemba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza katika ufunguzi wa mkutano wa 24 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP24 huko Katowice, Poland hii leo na kutaja mambo makuu manne anayoamini ni muhimu ili kubadili mwelekeo wa sasa wa tabianchi.

Bwana Guterres amesema mambo hayo manne ni muhimu kwa kuzingatia kuwa licha ya kushuhudia athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi duniani bado hatua za kutosha hazijachukuliwa kukabiliana na mabadiliko hayo.

Guterres ametaja mambo hayo kuwa ni mosi kwamba sayansi inataka hatua za juu zaidi ili kukabili athari hizo, ikizingatiwa kuwa kiwango cha hewa ya ukaa hewani kwa mujibu wa shirika la hali ya hewa duniani, WMO ni cha juu zaidi kuwahi kufikiwa katika miaka milioni 3 iliyopita.

Pili mkataba wa Paris ambao amesema unaweka mpango wa kuchukua hatua na hivyo ni lazima uanze kutekelezwa akisema “kazi yetu hapa Katowice ni kuhitimisha mpango wa utekelezaji wa mkataba wa Paris, au kanuni za utekelezaji.”

Ametaja hatua ya tatu ni kuwa ni  “tuna wajibu wa pamoja kuwekeza katika hatua za kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi, kuchangicha fedha kusaidia jamii zilizo hatarini,” akiongeza kuwa kuweka maendeleo dhahiri juu ya kuchangisha dola bilioni 100 kwa mwaka kutatoa ishara muhimu ya kisiasa inayohitajika.

Ujumbe wake wa nne ni kwamba hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zinatoa fursa bora  ya kubadili dunia iwe pahala bora zaidi.

Amekamilisha kwa kusema kuwa bado matumaini yapo akisema “ni lazima tuanze leo kujenga kesho tunayotaka. Hebu tukabiliane na changamoto na tukamilishe jukumu ambalo dunia inataka tutimize.”

VIONGOZI WENGINE KUTOKA COP24

Katika hotuba yake waziri mkuu wa Fiji, Frank Bainimarama, alliyekuwa rais wa COP23, akirejelea wito wa Katibu Mkuu ametolea wito mataifa ya ulimwengu kuwekeza juhudi mara tano zaidi, kuimarisha hatua mara tano zaidi na kuepuka kuwa “kizazi kitakachosaliti ubinadamu.”

Naye rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa, ameomba kuwepo kwa ujasiri katika hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kubainisha kuwa ushirikiano wa kimataifa ndio  njia pekee ya kuleta mabadiliko  ya athari mbaya za  joto duniani.

Kwa upande wake,rais wa COP24, Michal Kurtyka, amekumbushia hali ya  zamani ya  uchimbaji wa madini Katowice na kuwataka wajumbe  kufuata mwelekeo wa dhati na haki wakati wa kutekeleza mkataba wa paris. Awali rais wa Poland, Andrej Duda,aliwasilisha  “tamko la mabadiliko yenye kuzingatia haki .”

Benki ya dunia haikuachwa nyuma. Kupitia Afisa mwandamizi, Kristalina Georgiewa, imeaahidi kuongeza maradufu azma ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi baada ya 2020 kwa kuweka fungu la dola bilioni 100, ambapo nusu yake itatengwa kwa ajili ya kukabiliana na kustahimili mabadiliko ya tabianchi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter