Tufanye kazi kwa pamoja kutimiza haki kwa watu wenye ulemavu-Guterres

3 Disemba 2018

Zaidi ya watu bilioni moja duniani wana aina fulani  ya ulemavu na katika jamii nyingi, watu hao wanatengwa, wanakabiliwa na upweke na unyanyapaa.

 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa siku ya watu wenye ulemavu duniani inayoadhimishwa kila mwaka Disemba 3.

Guterres amesema tamko la kutomuacha mtu yeyote nyuma, la ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu linaashiria dhamira ya kupunguza kutokuwepo na usawa na kuimarisha ujumuishaji kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa watu wote, ikiwemo wanaoishi na ulemavu.

Hivyo amesema ni lazima kutekeleza mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika muktadha wote na nchi zote na kujumuisha pia sauti zao na wasiwasi wao katika ajenda na sera za kitaifa.

Ni kwa mantiki hiyo amesema Umoja wa Mataifa umezindua ripoti yake leo kuhusu ulemavu na maendeleo 2018- kufikia malengo ya maendeleo endelevu na, na kwa ajili ya watu wenye ulemavu. 

Ameongeza kuwa ripoti inaonesha watu wanoishi na ulemavu wako katika hali mbaya ukizingatia malengo mengi ya SDGs, lakini pia imetanabaisha hatua mujarabu ambazo zinaweza kujenga jamii jumuishi zaidi ili waweze kuishi kwa kujitegemea.

Katibu Mkuu huyo ametoa wito katika siku ya leo kwa kila mmoja kuonesha dhamira ya kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya dunia bora ambayo ni jumuishi, yenye usawa na endelevu kwa kila mtu, ambako haki za watu wenye ulemavu zinazingatiwa kikamilifu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter