Shime kila mtu apime UKIMWI: Guterres

Siku ya UKIMWI duniani ilianza kuafdhimishwa katika Makao Makuu ya UN New York miaka 13 iliyopita ! Disemba 1988.
UN Photo/Pernaca Sudhakaran
Siku ya UKIMWI duniani ilianza kuafdhimishwa katika Makao Makuu ya UN New York miaka 13 iliyopita ! Disemba 1988.

Shime kila mtu apime UKIMWI: Guterres

Afya

Miaka 30 tangu kuanza kwa maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani, harakati dhidi ya ugonjwa huo bado ziko njiapanda.

Hivyo ndivyo ameanza ujumbe wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika maadhimisho ya siku ya  Ukimwi duniani hii leo, Disemba Mosi,  maudhui yakiwa ishi kwa matumaini, fahamu hali yako.

Guterres amesema hali ni njiapanda kwa kuwa mtu mmoja kati ya watu wanne waishio na Virusi Vya Ukimwi, VVU  duniani hawafahamu iwapo wana virusi hivyo au la licha ya hatua kubwa zilizopigwa katika kuzuia  maambukizi.

Bw Guterres, ameendelea  kuwa  zaidi ya watu milioni 77 wameambukizwa VVU, ilhali wengine zaidi ya milioni 35 wamefariki dunia kutokana na maradhi yenye uhusiano na UKIMWI.

Kijana barubaru akifanyiwa vipimo vya Virusi vya UKIMWI huko nchini Ivory Coast
UNICEF/Frank Dejongh
Kijana barubaru akifanyiwa vipimo vya Virusi vya UKIMWI huko nchini Ivory Coast

 

Ni kwa kuzingatia mazingira hayo ya njiapanda, Guterres anasema upande ambao dunia itaamua kugeukia, utaashiria iwapo ni mwelekeo wa kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, au mwelekeo wa vizazi vijavyo kubeba mzigo wa gonjwa hilo hatari.

Hata hivyo amesema kuna matumaini kwa kuwa mamilioni kadhaa ya watu wameepuka maambukizi ya VVU kutokana na juhudi kali za upimaji, matibabu na kinga.

Katibu Mkuu amesema ingawa hivyo maendeleo hayo hayaendani na kile dunia inachotaka, kwani maambukizi mapya hayapungui kwa kasi inayotegemewa.

Kwa nini kasi ya kupungua maambukizi ni polepole?

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaja sababu kadhaa ikiwemo fedha zinazotakiwa katika harakati dhidi ya maambukizi kuwa hazitoshi na hivyo kuyafanya baadhi ya maeneo kubaki nyuma.

Pia unyanyapaa na ubaguzi kwa wagonjwa hali ambayo amesema inawazui watu au makundi kama vile  wanaoshiriki katika mapenzi ya jinsia moja, machangudoa, waliobadilisha jinsia, watumiaji madawa ya kulevya, wafungwa , na wahamiaji kujitokeza kupata matibabu.

Moise Maciel da Silva,19,kutoka Sao Paulo, Brazil, aligundua anaishi na VVU alipohitimu miaka 18.
© UNICEF/Danielle Pereira
Moise Maciel da Silva,19,kutoka Sao Paulo, Brazil, aligundua anaishi na VVU alipohitimu miaka 18.

 

Guterres amekamilisha ujumbe wake akiwatia moyo watu akisema muda bado upo kuwawezesha watu zaidi kupata matibabu, kuongeza fedha za kuzuia maambukizi mapya na pia kukomesha unyanyapaa akisema wakati huu mgumu ni heri kuchukua mwelekeo sawa.