Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya 60,000 hawasomi, vita vikifunga robo tatu ya shule Hudaydah:

Mtoto akisubiri mjini Hudaydah yemen wakati UNICEF ikigawa msaada wa nchini Yemen June 2018
UNICEF
Mtoto akisubiri mjini Hudaydah yemen wakati UNICEF ikigawa msaada wa nchini Yemen June 2018

Watoto zaidi ya 60,000 hawasomi, vita vikifunga robo tatu ya shule Hudaydah:

Utamaduni na Elimu

Watoto zaidi ya 60,000 wavulana kwa wasichana hawasomi kwa ajili ya mapigano ndani na katika viunga vya mji wa Hudaydah nchini Yemen.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto nchini humo UNICEF machafuko yamelazimisha Zaidi ya robo tatu ya shule kufungwa  ambapo shule 15 zipo msitari wa mbele na zingine kutokana na kusambaratishwa na viau au kutumika kama malazi kwa ajili ya familia za wakimbizi wa ndani.

Meritxell Relano mwakilishili wa UNICEF nchini Yemen akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis amesema hata zille shule ambazo zinaendelea na masomo imebidi zifanye hivyo kwa awamu tofautitofauti na kupunguza muda wa kufundisha uwe saa za asubuhi pekee.Ameongeza kuwa “katika eneo lililoathirika vibaya na vita la Hudaydah, mtoto mmoja tu kati ya watatu niye anayeweza kuendelea na elimu na chini ya robo ya waalimu wote ndio wanaopatikana shuleni. Wafanyakazi wengi katika sekata ya elimu Yemen hawajalipwa mishahara kwa zaidi ya miaka miwili na wengi wamelazimika kufungasha virago kukimbia machafuko au kwenda kusaka fursa nyingine ili kujipatia riziki.”

Ameongeza kuwa licha ya changamoto nyingi zinazowakabili waalimu kote Yemen bado wanaendelea kufundisha watoto katika njia wawezayo, dhamira yao ya kuendelea kuelimisha watoto nchini humo ni kitendo cha kishujaa. Amesisitiza kuwa “

“hakuna sehemu yoyote ya maisha ya watoto ambayo haijaathiriwa na vita nchini Yemen. Wakati vita kujeruhi na kukatili maisha ya watoto nchini Yemen , machafuko hayo pia yameathiri vibaya elimu ya watoto na matarajio ya mustakabali wao . Pande zote kinzani katika mzozo huu ni lazima zisitishe mara moja na kujizuia na operesheni zozote za kijeshi ndani na katika shule za na yemen nzima , ili kuwalinda wanafunzi, waalimu na wafanyakazi wengine katika sekta ya elimu na kutoa fursa ya elimu kwa mamilioni ya watoto nchini humo.”

Hivi sasa UNICEF inashughulikia program ya kuwapa waalimu fedha kidogo kila mwezi ili kuwawezesha kuendelea kufundisha hadi pale mgogoro wa mishahara utakapotatuliwa.