Sera za serikali zapora walalahoi haki ya nyumba, G20 chukueni hatua - Mtaalamu

29 Novemba 2018

Mkutano wa kundi la nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani, G20 ukianza kesho huko Buenos Aires nchini Argentina, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametaka viongozi hao kupatia suluhu janga la makazi ambalo linawanyima mamilioni ya watu ulimwenguni haki yao ya msingi ya kibinadamu.

“Yaonekana kuwa serikali kote ulimwenguni zimekumbwa na gonjwa la kupoteza kumbukumbu juu ya kile kilichochochea janga la kifedha mwaka 2008. Miaka 10 baada ya mzozo huo wa kiuchumi, viongozi wa G20 bado hawajashughulikia tatizo la makazi ambalo lilikuwa kitovu cha mzozo wa kifedha na tangu wakati huo hali imekuwa mbaya,” amesema Leila Farha, mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makazi.

Mtaalam huyo amesema ni vigumu sana kwa mtu kuona kuwa uchumi wa dunia ni tulivu ilhali mamilioni ya watu, hususan katika nchi wanachama wa kundi hilo na kwingineko  wanahaha kupata makazi bora ambayo wanaweza kumudu gharama zake na kuishi.

“Robo ya wakazi wa mijini duniani wanaishi kwenye makazi duni,” ametoa mfano Bi. Farha akisema kuwa ukosefu wa utulivu wa kiuchumi umesababishwa na taratibu mpya za mwenendo wa dunia ambazo zimechukulia makazi kama bidhaa na mbinu ya kifedha ya kukuza mtaji.

Viongozi wa kundi la nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani, G20 waomba kusaka suluhu ya janga la makazi, mfano ni pichani huko Tianjin, China, kuna tofauti kubwa ya makazi ndani ya miji.
World Bank/Yang Aijun
Viongozi wa kundi la nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani, G20 waomba kusaka suluhu ya janga la makazi, mfano ni pichani huko Tianjin, China, kuna tofauti kubwa ya makazi ndani ya miji.

Amesema viongozi wa G20 ni lazima wahakikishe kuwa watendaji wa kifedha na serikali zao wanazuia kuuzia watu watu wenye fedha nyingi, haki ya msingi ya binadamu ya kupata nyumba.

“Badala ya kujenga makazi ya kuishi, nyumba zinajengwa za kiana ili kukidhi mahitaji ya wawekezaji ambao bila shaka hawana nia ya kuishi eneo hilo. Biashara ya nyumba za makazi hivi sas ni biashara ya juu zaidi duniani ikikadiriwa kuwa na thamani ya dola trilioni 163—mara mbili zaidi ya thamani ya pato la ndani duniani,” amesema mtaalam huyo.

Ameonya kuwa maghorofa na nyumba za makazi si bidhaa kama mafuta na dhahabu, na badala yake makazi ni haki ya msingi ambazo hivi sasa serikali kupitia miundo ya kodi, sera na kanuni zimegeuza biashara kubwa inayoengua walala hoi.
 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter