Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yapeleka vifaa tiba katika eneo lililoathirika zaidi kwa mafuriko nchini Iraq.

WFP na washirika wake wamewahi kutoa msaada wa chakula katika mji wa Shirqat, kilomita 80 kusini mwa Mosul.
WFP MENA
WFP na washirika wake wamewahi kutoa msaada wa chakula katika mji wa Shirqat, kilomita 80 kusini mwa Mosul.

WHO yapeleka vifaa tiba katika eneo lililoathirika zaidi kwa mafuriko nchini Iraq.

Msaada wa Kibinadamu

Taarifa ya Shirika la Afya Ulimwenguni WHO iliyotolewa leo mjini Baghdad Iraq imesema dawa za kuokoa maisha na vifaa tiba vingine vimewasilishwa katika hospitali ya Shirqat kama sehemu ya kuwatibu walioathiriwa na mafuriko.

 

Mafuriko yaliyokumba eneo la Shirqat yaliacha uharibifu mkubwa wa mali, afya na miundombinu kama barabara, maji na umeme.

Shehena hiyo ya vifaa vya matibabu kutoka WHO ina zaidi ya tani 13 za dawa vikiwemo vikasha vinane vya kusaidia kutibu waliokumbwa na viwewe, ilhali vingine ni kwa ajili ya  upasuaji na dawa nyinigine kwa ajili ya kuweza kuwafanyia matibabu watu elfu 10 kwa kipindi cha miezi mitatu.

Kaimu mwakilishi wa WHO nchini Iraq Dkt. Adham Ismail akizungumzia msaada huo amesema, “ WHO imejizatiti kusaidia wizara ya afya na mamlaka za tiba katika eneo hili ili kutoa huduma za tiba kwa wenye uhitaji kote nchini Iraq. WHO pamoja na wadau wake wa afya bado wanahitaji kuingilia kati zaidi na kuhakikisha uwepo na urahisi wa kuzifikia huduma za kiafya ikiwemo rufaa, huduma za kiafya za papo kwa papo katika kambi na maeneo yaliyo mbali na vile vile sehemu ambazo ni vigumu kuzifikia”

Aidha taarifa ya WHO imeongeza kuwa katika eneo la Salah Eldin, zaidi ya nyumba 1000 zilisombwa na maji na kusababisha kuhamishwa kwa zaidi ya wakazi 5000 wa Shirqat ambao ndiyo waliuathiriwa zaidi.

Taarifa ya WHO imesema pia kuwa ingawa mamlaka zinazosimamia afya katika eneo hilo ziliripoti vifo 8, majeruhi 20 na idadi ambayo haijafahamika ya wasifahamika waliko, hali ya afya katika eneo hilo la Shirqat sasa inaendelea kudhibitiwa vizuri. Kliniki ya WHO ambayo inazunguka pamoja na magari ya wagonjwa yalitumwa mara tu baada ya mafuriko ili kuanza kutoa huduma kwa waathirika. Wengine walitibiwa na kurejea nyumbani na wengine walilazimika kupewa rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Ingawa hakuna magonjwa yasiyo ya kawaida ambayo yameripotiwa, WHO imewataka watoa huduma za kiafya katika maeneo mbalimbali kuendelea kufuatilia magonjwa ya kuambukiza kupitia tahadhari iliyotolewa mapema na shirika hilo la afya duniani.