Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani zaidi kupelekwa jimbo la Nile Magharibi

Maafisa wa kikosi cha polisi wanawake kutoka Rwanda wakitoa usaidizi kwa kuwatembelea maafisa wenzao waliokwenda kwenye kambi kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na watoto wanaoishi kwenye kituo cha ulinzi wa raia Juba , Sudan Kusini
Picha na UNMISS
Maafisa wa kikosi cha polisi wanawake kutoka Rwanda wakitoa usaidizi kwa kuwatembelea maafisa wenzao waliokwenda kwenye kambi kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na watoto wanaoishi kwenye kituo cha ulinzi wa raia Juba , Sudan Kusini

Walinda amani zaidi kupelekwa jimbo la Nile Magharibi

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema walinda amani zaidi kutoka chombo hicho watapelekwa kwenye jimbo la Nile Magharibi huko Sudan Kusini ili kufanikisha urejeshaji wa raia waliokimbia kutokana na mapigano. 

Helikopta ya Umoja wa Mataifa ikitua huko Kodok jimbo la Nile Magharibi nchini Sudan Kusini, ugeni ni mwakilishi wa kudumu wa Katibu Mkuu wa umoja huo nchini Sudan Kusini, David Shearer.

Ziara hii kwenye eneo hili muhimu lililopo kando mwa mto Nile inafanyika kukagua hali halisi hususan ya wakimbizi wa ndani ambao walifurushwa makwao baada ya mapigano.

Tayari walinda amani 40 wapo hapa Kodok kwa miezi saba sasa lakini Bwana Shearer anasema idadi yao itaongezwa ili kusaidia familia za wakimbizi wa ndani kurejea na pia kuimarisha hali ya kibinadamu.

“Inamaanisha pia mashirika ya kibinadamu nayo yanaweza kurejea. Na huko Kodog na Fashoda kwa ujumla, kuna umuhimu wa kuimarisha huduma za afya pamoja na miundombinu ya elimu.”

Image
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer.(Picha:UNMISS)

Katika ziara hii Bwana Shearer amekutana ndugu wawili, Regina na Sunday ambao hutumia saa mbili juani kufika shuleni, lakini mchana wakiwa wanarejea nyumbani huuza maziwa sokoni ili waweze kusaidia familia zao.

Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS amesema wahandisi wa ujumbe huo nao watasaidia kujenga miundombinu ya maeneo hayo, ikiwemo barabara na madaraja pamoja na kuimarisha gati.

Kuimarika kwa amani Kodok, kunathibitishwa na kushamiri kwa biashara ambapo wafanyabiashara wadogo wanasema kila siku watu zaidi wanarejea na idadi itakuwa kubwa wakati wa msimu wa kiangazi. Nyiker Okoth Awin, ni Naibu Gavana wa mji wa Fashoda.

“Hali ya  usalama ni nzuri na inaimarika, na bila shaka uwepo wa Umoja wa Mataifa, hususan walinda amani unaleta utulivu miongoni mwa watu kwasababu pindi wanapoona majeshi yasiyoegemea upande wowote, watu wanahisi kuna ulinzi, kando ya ulinzi tunaopatiwa na serikali. Wengine wanaweza wasiwe na sisi, kwa hiyo kuwepo na upande wa tatu ni jambo zuri."

Na kwa Mijok Albino, kutoka shirika la wanawake kwa amani Sudan Kusini, yeye ni maombi..

“Natumai amani itarejea na naendelea kuombea amani ili niweze kurejea nyumbani na kuanza tena maisha jimboni Fashoda"