UNICEF yaingiwa hofu juu ya hali ya watoto wahamiaji mpakani mwa Mexico na Marekani
UNICEF ina wasiwasi mkubwa juu ya usalama na ustawi wa zaidi ya watoto wahamiaji 1,000 walioko kwenye msafara huko Mexico au wakisubiri huko eneo la mpakani la Tijuana wakati huu ambapo madai yao ya kusaka hifadhi yakishughulikiwa na mamlaka za Marekani.
Hivyo ndivyo ilivyoanza taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa hii leo mjini New York, Marekani ikisema kuwa watoto hao wana fursa finyu ya kupata huduma za msingi ikiwemo lishe, elimu, matibabu na zile za kisaikolojia.
Taarifa hiyo imesema watoto hao wako hatarini pia kukumbwa na ukatili, uteswaji na hata kusafirishwa kiharamu wakati wakiwa kwenye msafara huo barabarani au wakiwa kwenye kambi za hifadhi zilizojaa pomoni.
“Mazingira hayo magumu wanakumbana nayo baada ya kukimbia ghasia, mateso, umaskini uliokithiri huko walikotoka kwenye nchi zao za kaskazini mwa Amerika ya Kati,” imesema taarifa hiyo.
“Kwanza mtoto ni mtoto, bila kujali hali yake ya uhamiaji. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, UNICEF inasihi serikali zote kuwapa hakikisho la hifadhi watoto wote waliofurushwa kutokana na madhila na wapatiwe hifadhi bila kuchelewa bila kujali wameingia vipi kwenye nchi husika,” imesema taarifa hiyo.
Halikadhalika taarifa imesema UNICEF inasihi serikali kwenye ukanda huo wa Amerika ya Kati kuhakikisha familia zinakuwepo pamoja na kutumia maeneo mbadala badala ya kuwasweka ndani katika vituo vya kuhifadhi wahamiaji.
“Vituo vya kusubiria vya uhamiaji na kusweka ndani wanafamilia ni kitendo kinachosababisha kiwewe na kinaweza kuacha watoto wakiwa katika mazingira hatarishi ya kutumikishwa au kuteswa,” imesema ripoti hiyo.
Pamoja na hiyo wametaka serikali zirejelee hatua za kuhakikisha zinashughulikia chanzo cha uhamiaji usiofuata kanuni, sababu ambazo ni pamoja na umaskini, ghasia na ukosefu wa fursa za kiuchumi na elimu na kwamba UNICEF iko tayari kushirikiana na serikali kwenye ukanda huo kuhakikisha watoto hao waliokimbia makwao wanapatiwa huduma na usaidizi unaohitajika.