Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa nchi za kusini kiungo muhimu katika kufanikisha SDGs-Guterres

Maendeleo endelevu ndio mkazo wa Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Cia Pak
Maendeleo endelevu ndio mkazo wa Umoja wa Mataifa.

Ushirikiano wa nchi za kusini kiungo muhimu katika kufanikisha SDGs-Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu, SDGs, haiwezi kufikiwa bila mchango wa nchi za kusini na ukweli upo dhahiri.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika hotuba yake kwa washiriki wa kongamano la ushirikiano baina ya nchi za kusini kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York,Marekani leo.

Bwana Guterres amesema nchi za kusini zimechangia kwa kiwango cha zaidi ya nusu cha maendeleo duniani katika miaka ya hivi majuzi, “huku biashara miongoni mwa nchi za kusini ni ya viwango vya juu ikiwa ni zaidi ya robo ya biashara kote ulimwenguni. Uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja ni wa juu zaidi kuliko wakati mwingine ikiwa ni theluthi ya uwekezaji duniani.”

Kama hiyo haitoshi, Katibu Mkuu amesema fedha zinazotumwa nyumbani na wafanyakazi wahamiaji kwa nchi za kipato cha chini na wastani zilifika dola bilioni 466 mwaka 2017 na kusaidia kuwanyanyua mamilioni ya watu kutoka katika lindi la umaskini.

Halikadhalika amesema mbinu mpya zinazoongozwa na nchi za kusini za kusambaza taarifa, teknolojia, kukabiliana na majanga na kuinua mapato zinabadilisha maisha.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo ametoa angalizo akisema, “ninaamini ushirikiano wa nchi za kusini kama kiungo muhimu cha kutekeleza ajenda ya 2030 kwa ajili ya ukuaji sawa, lakini ushirikiano wa nchi za kusini sio kwa ajili ya kuchukua nafasi ya ushirikiano wa nchi za Kaskazini na Kusini  na lengo lake sio kutishia makubaliano yaliyofikiwa kutokana na mpango wa Addis Ababa wa kuchukua hatua wa nchi za Kaskazini. Ushirikiano wa nchi za kusini ni kiungo muhimu lakini haupaswi kuchukua majukumu ya nchi za Kaskazini kwa ajili ya kutimiza ajenda ya 2010 na maendeleo ya kitaifa.”

Bwana Guterres amesema licha ya fursa zilizopo lakini wakati huohuo maendeleo hayajakuwa sawa na timilifu kwani asilimia 10 ya watu wanaishi katika umaskini uliokithiri licha ya hatua zilizopigwa katika baadhi ya maeneo, huku mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usawa ukichangia katika changamoto hizo. 

Katibu Mkuu huyo ametolea wito wadau kuchukua fursa katika kongamano hilo la siku nne na kubadilishana mawazo kuhusu mbinu za kudumu za kuleta mabadiliko katika nchi za kusini.

Ameziasa nchi kushirikiana kupiga hatua kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kuweka mipango inayolenga wanawake na kuimarisha fursa kwa vijana ili kufanikisha ushirikiano wa nchi za kusini kwa ajili ya watu wake na kwa ajili ya dunia mzima.