Pengo la ufadhili linahatarisha maisha ya watoto milioni 1 Mashariki ya kati:UNICEF

27 Novemba 2018

Takribani watoto milioni moja wa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wako hatarini wakati huu ambapo msimu wa baridi kali unanyemelea eneo hilo. Kutokana na hali hiyo ambayo watoto hao wanahitaji msaada wa haraka, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa ombi la dola milioni 33 ili kufikisha misaada.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa mjini Amman, Jordan, UNICEF inasema endapo haitapata msaada huo haraka  watoto hao watapata tabu wakati wa baridi kali ambapo fedha hizo zikipatikana zitatumika kuwanunulia nguo za kuleta joto, blanketi, maji na vifaa vya kujisafi.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika Geert Cappelaere, amesema kuwa , mgogoro wa muda mrefu, kuhamahama, na kutokuwa na ajira vimezifanya familia nyingi kupungukiwa na hela.

Amesema kuwa uhaba wa chakula chenye lishe, huduma za kiafya, vimewafanya watoto kukonda na wako hatarini kupata magonjwa  ya njia ya hewa na bila msaada  wa kuwalinda dhidi ya baridi watoto hao watakabiliwa na hali ngumu.

Taarifa ya UNICEF inaendelea kuwa hali ya baridi pia itaziathiri familia nyingi ambazo zinaishi katika kambi zilizojaa pomoni  huku zikiwa hazina vifaa vya kutosha vya kuwakinga dhidi ya baridi kali.

Kwa mujibu wa UNICEF, watoto wawili walifariki dunia  katika kipindi cha baridi kali kilichopita walipokuwa wanajaribu kusalimisha maisha yao  kutoka Syria kwenye vita hadi Lebanon.

UNICEF katika kipindi chote cha baridi kali, inapanga kuwafikia watoto milioni 1.3 nchini Syria, Iraq, Jordan, Lebanon, Uturuki na Misri  kuweza kuwapa nguo za joto, blanketi, maji ,vifaa vya kujisafi na pia kutoa pesa taslimu kwa familia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter