Licha ya ghasia, waafghanistani wana ‘kiu’ ya amani- UNAMA

27 Novemba 2018

Mkutano wa kimataifa wa ngazi ya juu umeanza leo  huko Geneva, Uswizi ukilenga kuonyesha mshikamao na wakazi wa nchi hiyo iliyogubikwa na vita na pia kusaidia serikali katika harakati zake za kuchagiza maendeleo sambamba na amani na usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari mwanzoni mwa mkutano huo wa siku mbili, Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Toby Lanzer amesema kila mkazi wa Afghanistani ambaye amekutana naye anataka kukomeshwa kwa ghasia na amani ishamiri.

Amesema Umoja wa Mataifa utafanya kila iwezalo, kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa, akisema suala la amani litakuwa ni moja ya mijadala.

 “Mwaka 2019 itakuwa ni miaka 40, yaani miongo minne ya ukosefu wa utulivu nchini Afghanistan,” amesema Bwana Lanzer akiongeza kuwa “kwa idadi kubwa ya wananchi wa Afghanistan, wamekulia katika mazingira ya kuona mzozo kuwa ni sehemu ya maisha yao. Kwa hiyo utafahamu zaidi hili  kuliko mimi- kuna kubwa ya amani. Nimekutana na watu tu ambao wanataka ghasia zikome na kwa hiyo Umoja wa Mataifa utafanya chochote uwezalo kufanikisha hilo,” amesema Bwana Lanzer.

Moja ya malengo ya mkutano huo ambao unahudhuriwa pia na Rais Ashraf Ghani, wa Afghanistan na mtendaji mkuu wa serikali Abdullah Abdullah, pamoja na maafisa lukuki kutoka Urusi, Uturuki na Muungano wa Ulaya ni kusisitiza umuhimu wa maendeleo katika kusaka amani na usalama.

UNHCR/Andrew McConnell
Wakimbizi wa Afghan ambao walifanya uamuzi mgumu wa kuamua kurejea katika nchi ya Afghanistani baada ya kuwa wamekimbilia kwa miongo kadhaa katika nchi ya Pakistani.

 

Ni katika mkutano huu pia ambapo itakuwa ni fursa ya kupima kile ambacho kimefanikiwa Afghanistan baada ya jamii ya kimataifa kuahidi dola bilioni 15.2 kama sehemu ya mpango wa miaka minne ya nchi hiyo kuanzia  mwaka 2016.

 “Iwe ni amani, iwe ni usalama, iwe ni maendewleo, iwe ni biashara, vitu vyote vinapaswa kumilikiwa na raia wenyewe wa Afghanistan na wao ndio wawe viongozi,” amesisitiza Bwana Lanzer ambaye pia ni Naibu Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan,  UNAMA.

Wakati huu ambapo watu milioni 3.6 nchini humo hawana uhakika wa kupata kabisa chakula, Lanzer ameseam kilichopo ni hatua moja tu kabla ya kufikia baa la njaa, “hivi ndivyo ambavyo ukame umepiga mwaka huu wa 2018.”

Pamoja na kugawa chakula kwa wahitaji, kuwapatia malazi watu ambao wamekimbia makazi yao kutokana na njaa au wale wanaorejea Afghanistan, kimesalia kuwa kipaumbele cha dharura wakati huu ambapo majira ya baridi kali yanaanza.

 “Mwaka huu hadi sasa watu 675,000 wamerejea Afghstanin wakitokea Iran. Na wakati huo huo watu 500,000 wanalazimika kukimbia makazi yao humu nchini, kisa? Kutokana na ghasia zinazoendelea na ukame.” Amesema Lanzer.

Akizungumzia uchaguzi ambao, kuna madai kuwa utasogezwa mbele, Bwana Lanzer amesam hakuna mabadiliko ya tarehe ambayo wamepokea kutoka tume huru ya uchaguzi nchini humo.

“Tunafanya kazi kwa kuzingatia taarifa kuwa uchaguzi wa rais utafanyika tarehe 20 mwezi Aprili mwakani kama ilivyopangwa na hiyo tarehe ndio bado tunajadili na mamlaka, “ amesema Bwana Lanzer.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud