Afrika yalenga kurahishisha ufanyaji biashara kimataifa
Nchi za Afrika ambazo zinalenga kupunguza gharama, muda na urasimu wa kufanya biashara ya kikanda na kimataifa zinakutana kuanzia leo huko Addis Ababa, Ethiopia, katika warsha ya kwanza kabisa ya Afrika kwa ajili ya kuunda kamati za kuwezesha biashara.
Warsha hiyo ya aina yake ilioandaliwa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD na wadau inafanyika wakati huu ambapo bara la Afrika limeimarisha juhudi za kurahisisha ufanyaji biashara kufuatia makubaliano ya biashara ya shirika la biashara duniani, WTO na wakati ikisubiri kutekeleza makubaliano ya eneo huru la biashara barani Afrika, AfCFTA, yaliyotiwa saini mwezi Machi 2018.
Akizungumzia warsha hiyo Katibu Mtendaji wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema, WTO inakadiria gharama ya kufanya biashara katika mataifa yanayoendelea kuwa ni sawa na asilimia 219 ya ushuru kwa biashara ya kimataifa, hali ambayo inaathiri vibaya bara hilo.
Kwa mujibu wa UNCTAD lengo la warsha ni kuhakikisha kila nchi inaweka kamati ya taifa ya kusimamia biashara ikijumuisha sekta binafsi na ya umma kwa ajili ya kusimamia biashara nyumbani na kufuatilia makubaliano ya warsha.
Uwepo wa kamati hizo utawezesha kufanya biashara kwa gharama ndogo na kwa muda mfupi hususan katika mataifa yanayoendelea ambapo mengi yapo kusini mwa jangwa la Sahara.
UNCTAD imesema mabadiliko hayo yatawawezesha wafanyabiashara wadogo hususan wanawake kuingia katika sekta rasmi, yataimarsha shughuli za biashara na kuweka uwazi, kuimarisha usimamizi bora, yatatoa fursa bora za ajira na kuimraisha TEHAMA katika jamii na ni kiungo muhimu katika kuingia soko za kimataida na kuondokana na umaskini.
Warsha hiyo itakayowaleta pamoja wadau mbalimbali na mashirika ya kimataifa itamalizika tarehe 29 mwezi huu.