Jaribio jipya la dawa dhidi ya Ebola laanza tena DR Congo.

26 Novemba 2018

Shirika la afya duniani WHO leo limetangaza kuwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo inaanza kutoa dawa mpya ya majaribio. Dawa hii mkusanyiko wa dawa mbalimbali zenye lengo la kuunganisha nguvu dhidi ya virusi vya Ebola.

Wizara ya afya nchini humo imetangaza kuwa jaribio la la sasa limeanza ili pia kutathmini ufanisi na usalama wa dawa zilizotumika kuwatibu wagonjwa wa Ebola.

“Ni utafiti unaohusisha nchi nyingi ambao ulikubaliwa na washirika chini ya mpango wa Shirika la Afya Duniani” imesema taarifa ya WHO.

Akizungumzia hatua hii, Mkurugenzi  Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema “wakati bado lengo letu linabakia kuutokomeza ugonjwa huu, uanzishwaji wa matibabu haya ni hatua ya muhimu kuelekea hatimaye kupata tiba ya Ebola itakayookoa maisha. Hadi sasa wagonjwa wametibiwa kwa kutumia dawa ambazo zimeonesha matumaini. Hatua kubwa ambayo DRC inachukua hivi sasa italeta mwanga wa kipi kinafanya kazi sawasawa na kuokoa maisha ya wengi kwa miaka ijayo. Tuna matumaini ya siku moja kusema kuwa vifo na mateso ya Ebola yatakuwa nyuma yetu.”

Hadi sasa, zaidi ya wagonjwa 160 wametibiwa kwa kutumia matibabu ya uchunguzi chini ya mfumo wa maadili wa WHO kwa kushirikiana na wataalam wanaohusika na dawa za majaribio au zile ambazo hazijasajiliwa bado.

Waziri wa afya wa DRC Dkt. Olly Ilunga amesema, “nchi yetu imepigwa na milipuko ya Ebola ya mara kwa mara, jambo ambalo pia linamaanisha kuwa tuna utalaam wa kipekee wa kupambana nayo. Majaribio haya yatachangia katika kukuza uelewa wakati tunaendelea kupambana kuhakikisha mlipuko wa sasa unafikia ukomo”

Mwezi Oktoba mwaka huu, WHO iliitisha mkutano wa mashirika ya kimataifa, wadau wa Umoja wa Mataifa, nchi zilizoko katika hatari ya kushambuliwa na Ebola, watengenezaji wa dawa na wengine, ili kukubaliana katika namna ya kuendelea  na majaribio katika mlipuko mwingine wa Ebola popote utakakotokea.

Jaribio la sasa limeandaliwa na WHO, kuongozwa na kufadhiliwa Taasisi ya utafiti wa dawa ya DR Congo INRB ikishirikina na Wizara ya Afya ya nchi hiyo ntTaasisi ya kitaifa ya magonjwa ya mzio na kuambukiza NIAID, ikiwa ni sehemu ya Taasisi ya Taifa ya Marekani pamoja na mashirika mengine.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud